Wabunge watano wa Uingereza wamemwandikia barua waziri wao wa mambo ya nje Yvette Cooper wakiitaka serikali ya London “ifuatilie kwa dharura uingiliaji kati wa kijeshi utakaoongozwa na Umoja wa Mataifa” ili kukomesha mauaji ya kimbari ya yanayofanywa na Israel huko Ghaza.

Barua hiyo iliyoandaliwa na mbunge wa kujitegemea Adnan Hussain imetiwa saini na wanachama wenzake watatu wa Muungano wa wabunge wa kujitegemea – Ayoub Khan, Iqbal Mohamed na Shockat Adam – pamoja na Mbunge wa Liberal Democrat Andrew George.

Hatua hiyo inafuatia ripoti mpya ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina na Israel, ambayo imegundua kuwa utawala wa kizayuni wa Israel umefanya vitendo vinne kati ya vitano vilivyopigwa marufuku chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948, na kwamba viongozi wa utawala huo ghasibu walikuwa na nia ya kuwaangamiza Wapalestina kama jamii huko Ghaza.

“Uingereza ni mtia saini mwanzilishi wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” inasomeka sehemu moja ya barua hiyo ikiendelea kueleza: “nafasi hizi si za kiheshima tu. Zinafungamana na masharti ya kisheria na wajibu”.

Barua ya wabunge hao wa Uingereza inasema, Mkataba wa Mauaji ya Kimbari unailazimisha Uingereza “izuie na kuadhibu (wahusika wa) mauaji ya kimbari”.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Mkataba wa Umoja wa Mataifa “unaidhinisha Baraza la Usalama kuchukua hatua za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kuingilia kijeshi, katika kesi ambapo kuna tishio kwa amani na usalama wa kimataifa”.

Wabunge hao wanaitaka serikali ya Uingereza kuwasilisha azimio kwenye Baraza la Usalama “kuidhinisha hatua zote muhimu, ikiwa ni pamoja na hatua za kijeshi, kulinda raia huko Ghaza na kukomesha mauaji ya kimbari”.

Ikiwa azimio hilo litakwamishwa, -barua inasema-, Uingereza lazima iongoze mpango katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutafuta uingiliaji kati huko Ghaza utakaoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ili kuzuia mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni dhidi ya Wapalestina…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *