
Ismail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa na kusema kuwa, ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa haikubakisha chembe ya shaka kwamba jinai za Israel huko Ghaza ni mauaji ya kimbari, hivyo waungaji mkono wa utawala huo ghasibu wanapaswa kuacha kushiriki katika mauaji ya kimbari ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Baghaei ameandika hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X ikiwa ni kuonesha hisia zake kuhusu ripoti ya hivi karibuni ya “Kamisheni ya Uchunguzi ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa” iliyosema bila kificho kwamba jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza ni “mauaji ya kimbari.”
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imekuja kuyasuta madai ya Septemba 1 mwaka huu ya Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Uingereza David Lammy aliyedai katika barua yake kwa mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kimataifa ya Bunge la Kimataifa kwamba eti Israel haijawahi kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ameandika: “Tume Huru ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Uhalifu Uliofanywa na Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, inayoongozwa na mwanasheria maarufu Bi. Navi Pillay, sasa haikubakisha chembe ya shaka juu ya aina ya uhalifu na ukatili unaofanywa huko Ghaza.
Tume hiyo imesema wazi katika taarifa yake ya kurasa 72 kwamba Israel imefanya mauaji ya kimbari Ghaza tena kwa kutumia neno hilo hilo la “mauaji ya kimbari.” Amesema: “Wafuasi wa utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya umati lazima wabebe dhima ya kisheria na kimaadili na kuacha kushiriki katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.”