
Katika jitihada zake mpya za kuungwa mkono kimataifa wananchi wa Ghaza na wananchi wa Palestina kiujumla, harakati ya Hamas imetoa mwito kwa watu wote walio huru duniani kuzitangaza siku Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuwa siku za hasira za kimataifa dhidi ya Wazayuni wavamizi na wafuasi wao kupitia kukusanyika mbele ya balozi za nchi zote zinazoshiriki kwenye jinai za Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilitoa mwito huo jana Alkhamisi na kutaka kuimarishwa harakati za kimataifa za kuiunga mkono Ghaza.
Hamas imesema: tunatoa mwito wa kuendelezwa na kushadidishwa harakati za kimataifa za mshikamano na Ghaza katika kulaani hujuma za wavamizi na jinai za mauaji ya kimbari na njaa dhidi ya zaidi ya watu milioni 2 wa Ukanda wa Ghaza, na vile vile katika kukabiliana na jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni huko Ghaza, uharibifu mkubwa wa majengo unaofanywa na utawala wa Kizayuni.
Taarifa ya Hamas imesema: Siku za Ijumaa ya leo, Jumamosi na Jumapili, za Septemba 19, 20 na 21, zinapaswa kuwa siku za matembezi ya ghadhabu dhidi ya wavamizi na wafuasi wao, ziwe kilio dhidi ya ukimya na dharau ya kimataifa ya kushindwa kukomesha jinai za Israel na kuondolewa mzingiro wa Ghaza.
Vilevile taarifa hiyo ya HAMAS imesema: Tunatoa mwito kwa dhamiri zilizoamka na watu wote walio huru ulimwenguni kushiriki kikamilifu katika maandamano ya hasira mbele ya balozi za Israel na Marekani, pamoja na balozi za nchi zote zinazounga mkono jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni kwa shabaha ya kufichua jinai za mauaji ya kimbari na njaa ya raia katika Ukanda wa Ghaza na kutetea haki za watu hao kwa uhuru.