Mji mkuu wa Guinea, ulikuwa na shughuli nyingi jana Alkhamisi, ambayo ilikuwa siku ya kufunga kampeni kabla ya kufanyika kura ya maoni ambayo itaweza kumruhusu kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini humo miaka mitatu iliyopita kuwania urais.

Hafla za visomo vya Qur’ani na dua pamoja na matamasha ya muziki wa reggae yalifanyika kumuunga mkono Kanali Mamadi Doumbouya, kiongozi wa kijeshi aliyetwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi hayo.

Majengo ya umma na ya binafsi katika mji mkuu Conakry yalibandikwa mabango mbalimbali ya kampeni.

Barabara zilizibwa na malori yaliyojaa wafuasi waliovalia fulana na nguo za kiutamaduni zenye picha za Doumbouya.

Hata hivyo kampeni hizo zimekosa kitu kimoja cha msingi ambacho ni upinzani. Mabango na matukio yote ya kampeni hizo yanawahimiza watu kupiga kura kwa njia moja tu ya: “Ndiyo”.

Raia wa nchi hiyo ya pwani ya Afrika Magharibi wataipigia kura ya Ndiyo au Hapana siku ya Jumapili rasimu ya Katiba, ambayo ni hatua muhimu katika mabadiliko kutoka utawala wa kijeshi kuelekea utawala wa kiraia. Hakuna kampeni inayoruhusiwa kufanywa leo Ijumaa na kesho Jumamosi kabla ya zoezi hilo la siku ya Jumapili.

Uchaguzi wa urais wa Guinea unatarajiwa kufanyika mwezi Disemba. Kuna wapiga kura milioni sita na laki saba waliotimiza masharti, na kura hiyo ya maoni itahitaji kwa uchache 50% ya kura ili kuweza kupita…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *