Serikali ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban imetupilia mbali wito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka jeshi la nchi hiyo lirejee Afghanista na kupatiwa tena kambi ya jeshi la anga ya Bagram.

Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afghanistan, Zakir Jalal ametangaza kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa kwamba Kabul iko tayari kufanya mazungumzo na Washington, lakini amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusiwa kuanzisha tena uwepo wake wa kijeshi katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.

Jana Alkhamisi, Trump alisema serikali yake inashinikiza “irejeshewe” kituo cha Bagram. Rais wa Marekani, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akielezea matumaini ya kukipata tena kituo hicho, alibainisha kwambaa mahali ilipo Bagram ni muhimu kimkakati kutokana na ukaribu wake na China.

“Tunajaribu kuipata tena,” Trump alitangaza na kufafanua kwa kusema: “Tuliitoa kwa [Taliban] kupata chochote”, alilalama rais huyo wa Marekani na kuongeza kuwa Bagram “iko umbali wa saa moja tu kutoka mahali China inapotengeneza makombora yake ya nyuklia”.

Hata hivyo, maafisa wa Taliban wametupilia mbali wazo hilo.

“Afghanistan na Marekani zinahitaji kuzungumza… bila Marekani kudumisha uwepo wowote wa kijeshi katika sehemu yoyote ya Afghanistan,” ametamka bayana Jalal, katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii.

Aidha, amesema Kabul iko tayari kufuatilia suala la kuwa na uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na Washington kwa msingi wa “kuheshimiana na kuzingatia maslahi ya pamoja”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *