
Vyama vya wagombea wawili wakuu katika uchaguzi wa rais nchini Malawi vimejitangazia ushindi na kuzua wasiwasi wa kuibuuka mzozo.
Chama cha Rais Lazarus Chakwera cha Malawi Congress Party na kile cha Peter Mutharika cha Democratic Progressive vimetoa taarifa na kudai kuwa wagombea wao wameibuka na ushindi katika kiti cha urais.
Tume ya Uchaguzi wa Malawi imetangaza kuwa, tayari imehesabu asilimia 99 ya kura lakini haijatangaza rasmi matokeo huku ikikemea hatua ya vyama hivyo kujitangazia ushindi. Mwenyekiti wa tume hiyo Justice Annabel Mtalimanja amesema hawataharakisha mchakato wa kuhesabu kura akivitaka vyama na wagombea kuheshimu mchakato na taratibu za kutangaza matokeo.
Uchaguzi wa Malawi uliofanyika siku ya Jumanne ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Rais wa sasa wa Malawi Lazarus Chakwera na rais wa zamani Peter Mutharika, ambaye aliondolewa madarakani na Chakwera katika uchaguzi uliopita.
Kama hatopatikana mgombea atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, uchaguzi huo utaingia kwenye duru ya pili.
Malawi imekumbwa na mdororo wa kiuchumi tangu kiongozi wa kanisa, mchungaji Chakwera alipochaguliwa kuwa rais, mwaka 2020, huku kukiwa na kimbunga kikali na ukame ulioangamiza mazao na kupelekea hali ya maisha kuwa mbaya zaidi. Mfumuko wa bei umeongezeka kwa zaidi ya 20% tangu miaka mitatu iliyopita.
Kashfa za ufisadi zimechangia kukatishwa tamaa wananchi. Mchungaji Chakwera aliingia madarakani akiishutumu serikali ya zamani ya Mutharika kwa ufisadi uliokithiri, lakini hali imezidi kuwa mbaya alipoingia madarakani.
Kuna uwezekano mkubwa kwa chama chochote kitakachoshinda kati ya hivyo viwili vikubwa, kile cha mchungaji Chakwera cha Malawi Congress au cha Mutharika cha Democratic Progressive Party kitalazimika kuunda muungano na vyama vidogo ili kupata viti vingi bungeni.