
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa zaidi ya watoto 26,000 katika Ukanda wa Gaza wanahitaji matibabu ya haraka kutokana na utapiamlo mkali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Wafa la Palestina, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza katika ripoti yake kuwa zaidi ya watoto 26,000 katika Ukanda wa Gaza wakiwemo zaidi ya watoto 10,000 katika mji wa Gaza wanahitaji matibabu ya dharura kutokana na utapiamlo mkali.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina Wafa, mtoto mmoja kati ya wanane wanaochunguzwa katika Ukanda wa Gaza anaugua utapiamlo mkali, huku katika mji wa Gaza uwiano huu ukiongezeka hadi mmoja kati ya watano. Hiki ndicho kiwango cha juu zaidi cha utapiamlo kilichorekodiwa katika historia.
Vituo vya lishe huko Gaza, ambavyo vilikuwa na jukumu muhimu katika kutoa huduma kwa watoto wenye utapiamlo, vimefungwa kutokana na maagizo ya kuhama na kuongezeka kwa operesheni za kijeshi wiki hii.
UNICEF pia imesema kuwa ni unyama kuwataka watoto nusu milioni, ambao wameteseka kwa zaidi ya siku 700 za vita, kukimbia kutoka jahanamu moja hadi nyingine.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Taarifa ya UNICEF ya hivi karibuni ilisema kuwa, hali katika mji wa Gaza na katika Ukanda wote huo ni mbaya sana, bila chakula au dawa, na mbaya zaidi, watu wanajua kwamba hakuna msaada wa kweli wa kimataifa kwao, na hali itazidi kuwa mbaya zaidi.
Wakati huo huo, kufuatia kuenea kwa janga la njaa katika Ukanda wa Gaza, maonyo ya kimataifa kuhusu mzozo wa kibinadamu katika ukanda huo yanaendelea kuongezeka, na Tess Ingram, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), ameonya juu ya hali inayoongezeka ya njaa katika mji wa Gaza, na kusema kwamba ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, hatari hii itaenea katikati mwa Ukanda wa Gaza ndani ya wiki chache.