
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen huku akipuuzilia mbali vitisho vya waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni ametangaza kuingia kwa silaha mpya katika medani ya vita kati ya nchi ya Kiarabu na utawala haramu wa Israel pamoja na washirika wake wa Magharibi.
Hizam al-Assad, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema katika kujibu vitisho vya Yisrael Katz, Waziri wa Vita wa Israel kwamba: “Hatuogopi vitisho vya wavamizi na tumeleta silaha mpya katika medani ya vita.” Amelichukulia tishio la watawala wa Kizayuni la kumuua Sayed Abdul Malik al-Houthi, Katibu Mkuu wa Ansarullah ya Yemen kuwa ni ishara ya udhaifu na kutojiweza Israel.
Hizam al-Assad amekitaja tishio la kupeperushwa bendera ya Israel huko Sana’a kuwa ni kichekesho na kusema: ‘Vitisho vya Katz vya kunyanyua bendera ya utawala wa Israel juu ya Sana’a, mji mkuu wa Yemen, ni kichekesho na wala hataweka mguu wake Sana’a. Msimamo wetu ni thabiti katika kuunga mkono muqawama huko Gaza hadi vita vya mauaji ya halaiki vitakaposimama.’
Ansarullah ya Yemen imekuwa akionyesha msimamo thabiti na wa kishujaa katika kukabiliana moja kwa moja na utawala wa Kizayuni na Israel na washirika wake wa Magharibi ikiwa ni katika kuwatetea watu wanaodhulumiwa na kukandamizwa na utawala huo huko Gaza.