
Ufaransa imeamuru wanadiplomasia wawili wa Mali kuondoka nchini humo, kufuatia kukamatwa kwa mwanadiplomasia wake nchini Mali mwezi Agosti.
Kwa mujibu wa chanzo cha kidiplomasia cha Ufaransa kilichonukuliwa na AFP, maafisa hao wawili wa Mali wametangazwa kuwa “watu wasiotakikana” na wameagizwa kuondoka Ufaransa kufikia leo Jumamosi.
Chanzo hicho pia kimeonya kuwa “hatua nyingine” zinaweza kuchukuliwa endapo raia wa Ufaransa aliyekamatwa hataachiliwa haraka.
Mgogoro huo unatokana na kukamatwa kwa mfanyakazi wa ubalozi wa Ufaransa mjini Bamako tarehe 15 Agosti. Mamlaka za Mali zinamtuhumu Yann Vezilier kuwa jasusi wa mashirika ya ujasusi ya Ufaransa ambapo amekuwa akijaribu kuwachochea wanasiasa, wanaharakati wa kijamii na maafisa wa kijeshi wakiwemo majenerali Abass Dembele na Nema Sagara “kuvuruga utulivu wa serikali ya Mali.”
Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Mali, Daoud Aly Mohammedine, Vezilier alikuwa miongoni mwa “kikundi kidogo cha wachochezi waliotengwa” ndani ya jeshi la Mali.
Ufaransa imekanusha vikali tuhuma hizo na kusema mazungumzo na maafisa wa Mali yanaendelea kwa lengo la “kuondoa hali ya kutoelewana na kuhakikisha kuachiliwa mara moja” kwa mfanyakazi wake.
Mwezi Agosti, Waziri wa Usalama wa Mali Daoud Aly Mohammedine alisema uchunguzi unaendelea kubaini “wasaidizi wa ndani” katika “vitendo vya uchochezi” dhidi ya Bamako unaohusisha “mataifa ya kigeni,” kufuatia kukamatwa kwa Vezilier na wanajeshi kadhaa wa Mali.
Mahusiano kati ya Ufaransa na Mali yamezorota sana katika miaka ya hivi karibuni. Muungano wa Nchi za Sahel (AES) , ulioundwa na Mali, Burkina Faso, na Niger, umekuwa ukishutumu mara kwa mara Ufaransa kwa kujaribu kuuvuruga muungano huo kwa kuwashinikiza wanachama wake kusalitiana.
Kiongozi wa mpito wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tchiani, amedokeza kuwa maafisa wa Ufaransa pia wanashirikiana na makundi ya waasi katika maeneo ya mpakani ya Benin na Nigeria kama sehemu ya mpango wa pamoja wa kuleta machafuko nchini mwake na katika ukanda mzima wa Sahel.