Ajali mbili za baharini karibu na pwani ya Libya zimeacha zaidi ya wakimbizi 110 wa Kisudan wakiwa wamefariki au hawajulikani walipo, kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi  (UNHCR) nchini Libya limethibitisha kuwa chombo kilichokuwa na watu 74 kilizama Jumamosi iliyopita karibu na pwani ya mji wa Tobruk mashariki mwa Libya. Ni watu 13 pekee walionusurika, huku wengine wengi wakiwa hawajulikani walipo. UNHCR imeeleza kuwa waathirika wengi walikuwa wakimbizi wa Kisudan waliokuwa wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti ajali nyingine iliyotokea Jumapili. Kwa mujibu wa IOM, takriban watu 50 walifariki baada ya boti iliyokuwa na wakimbizi 75 wa Kisudan waliokuwa wakielekea Ugiriki kushika moto karibu na pwani ya Libya. Shirika hilo limesema liliwapatia huduma ya dharura ya matibabu manusura 24.

Raia wa Sudan kwa sasa wanawakilisha idadi kubwa ya wale wanaojaribu safari hatarishi kuvuka Mediterania. Harakati zao zinasababishwa na mzozo unaoendelea nchini Sudan ambao umesabishwa na mapigano kati ya waasi wa RSF na Jeshi la Sudan (SAF) yaliyoanza Aprili 2023. Umoja wa Mataifa umeutaja mzozo huo kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani, likiwa limesababisha maelfu ya vifo na mamilioni ya watu kutawanywa.

Alhamisi iliyopita, UNHCR katika Afrika Magharibi na Kati iliripoti kuwa zaidi ya wakimbizi 877,000 wa Kisudan wamekimbilia Chad tangu kuzuka kwa machafuko. Mapema Septemba, shirika hilo lilitangaza kuwa takriban watu milioni 12 wamelazimika kuhama makazi yao nchini Sudan.

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa limeitaja Libya, ambayo bado ni njia kuu ya kupitisha wahamiaji wanaokimbia vita na umasikini kutoka Afrika na Asia Magharibi au Mashariki ya Kati, kuwa mojawapo ya njia hatari zaidi za kufikia Ulaya kwa njia ya bahari. Takwimu za IOM zinaonesha vifo 317 vilivyothibitishwa na watu 286 waliopotea katika njia ya Mediterania ya Kati kati ya Januari na mapema Agosti 2025. Katika kipindi hicho hicho, takriban wahamiaji 14,000 walinaswa baharini na kurejeshwa Libya na walinzi wa pwani, kwa mujibu wa Libya Review.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *