
Waasi wameshambulia mji mmoja wa mpakani katika jimbo la Borno, kaskazini mwa Nigeria na kuchukua silaha katika kambi ya kijeshi katika eneo hilo huku wanajeshi wakikimbilia usalama wao katika nchi jirani. Hayo yamesemwa na wakazi na maafisa wa usalama katika eneo la tukio. Tukio hilo limeripotiwa katika mji wa Banki, katika wilaya ya Bama.
Waasi wameimarisha shughuli zao katika eneo hilo katika siku za karibuni. Tukio la karibuni lilianza siku ya Alkhamisi na kumalizika masaa ya alfajiri Ijumaa.
Baada ya waasi kuvamia kambi hiyo ya jeshi, askari walikimbilia usalama wao katika nchi jirani ya Cameroon huku wakiwaacha raia bila usalama wowote. Askari mmoja alisema kwamba waasi waliwasili wakiwa katika kundi kubwa na hivyo kuwazidi nguvu wanajeshi baada ya makabiliano makali ya ufyatuaji risasi.
Wapiganaji wa Boko Haram waliteka mji huo wa Banki miaka kumi iliyopita, ambapo umekuwa ukiangukia mikononi mwa waiganaji tofauti wa makundi ya kigaidi na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa wa kiusalama na kiraia katika eneo hilo.
Jeshi la Nigeria limekuwa likidai kwamba limeimarisha operesheni zake katika eneo hilo la kakazini mwa nchi kwa ajili ya kukabiliana na waasi lakini ukweli wa mambo unaonyesha hali tofauti kabisa ya kiusalama nyanjani.