Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa notisi likisisitiza kuwa ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA utasitishwa hivi karibuni.
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa limesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kutokana na hatua zisizo za busara za nchi 3 za Ulaya kuhusiana na suala la nyuklia la Iran, na licha ya ushirikiano mzuri wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na pia kuwasilishwa mipango ya kutatua suala hilo.
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa pia limeeleza katika tangazo hilo kwamba, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepewa jukumu la kuendeleza mashauriano yake katika fremu ya maamuzi ya baraza hilo kwa ajili ya kulinda maslahi ya kitaifa ya nchi.
Kikao cha karibuni cha Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, chini ya uenyekiti wa Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kimesisitiza kuwa, siasa za Iran hivi sasa zitakuwa ni kushirikiana kadiri inavyowezekana na pande tofauti kwa ajili ya kuleta amani na utulivu katika eneo.
Kikao hicho pia kimejaili hatua za baadhi ya nchi katika uga wa kimataifa ambazo zimetekeleza operesheni za kijeshi na vikwazo na vile vile hatua zilizochukuliwa karibuni hivi na nchi 3 za Ulaya kuhusiana na suala la nyuklia la Iran.
Katika maingiliano yake ya karibuni na Troika ya Ulaya ambazo ni nchi za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza pamoja na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Iran imetoa matakwa yake halali na ya kimantiki, ambayo kimsingi yanalinda maslahi ya taifa, kuzingatia sheria za kimataifa na kuzuia kuongezeka mivutano katika kadhia ya nyuklia.
Iran inataka kuanzisha itifaki mpya ya ushirikiano na IAEA ambayo inaendana na mazingira mapya na mashambulizi ya hivi karibuni ya maadui dhidi ya vituo vyake vya nyuklia ambavyo vinaendeshwa kwa malengo ya amani. Iran inasisitiza kuwa, wakala huo unapaswa kuepuka kuingia katika michezo ya kisiasa ya Wamagharibi na kuchukua hatua kwa msingi wa majukumu yake ya kiufundi na kiusalama tu.

Ushirikiano wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na Wakala huo pia unapaswa kuwa ndani ya fremu ya sheria zilizoidhinishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge, na kwa kuzingatia usalama wa taifa. Iran pia inataka kusitishwa mara moja kwa hatua zisizo halali za nchi tatu za Ulaya za kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama, ambazo inazichukulia kutokuwa na uhalali wowote wa kisheria. Iran inasisitiza kuwa, fursa iliyobakia itumike kwa ajili ya kufikia makubaliano ya kiadilifu na usawa, na pande za Ulaya zijiepushe na ushawishi wa wachochezi wenye misimamo mikali.
Katika misimamo yake ya hivi karibuni, Iran imeonyesha kwamba inataka kuwa na mwingiliano wenye kujenga, kudumisha mifumo ya kisheria ya kimataifa na kuzuia kuongezeka mgogoro kuhusu kadhia yake ya nyuklia. Pamoja na hayo, inasisitiza kwamba ushirikiano wowote unapaswa kuzingatia misingi ya kuheshimiana, maslahi ya pamoja na kuepuka kujitakia makuu.
Matakwa ya Iran kutoka kwa Troika ya Ulaya na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki yanaonyesha jaribio la Tehran la kufafanua upya kanuni za mchezo katika uwanja wa diplomasia ya nyuklia. Matakwa haya si ya kiufundi na kisheria tu, bali pia yana matokeo muhimu ya kisiasa na kimkakati. Matakwa kama vile kusimamishwa utaratibu wa ‘snapback’ na IAEA kujiepusha na ushawishi wa kisiasa ni jaribio la kuzima makali ya chombo cha mashinikizo kinachotumiwa vibaya na nchi za Magharibi.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwasilisha ‘utaratibu mpya’ inataka kubadilisha nafasi ya wakala huo kutoka kuwa msimamizi mwenye mwelekeo tegemezi na wa upendeleo hadi mshirika wa kutegemewa kiufundi na kitaalamu. Mabadiliko haya yanaweza kupelekea kuongezeka uwazi katika shughuli za IAEA. Sisitizo la Iran la kutumia fursa iliyosalia kwa ajili ya kufikia makubaliano yanayofaa, unaonyesha nia yake ya kudumisha njia ya diplomasia. Matakwa ya Iran kwa Troika ya Ulaya na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki yanatokana na sheria za kimataifa na maslahi ya kitaifa ya Iran, na yanaweza kufufua njia ya diplomasia ikiwa pande nyingine husika zitajibu vizuri matakwa hayo.
Ili kufikia mwafaka kuhusu suala la nyuklia la Iran, ni lazima msururu wa hatua za pande kadhaa, zenye uwiano na za kujenga imani, zichukuliwe na kutekelezwa katika uwanja huo na upande wa pili yaani Troika ya Ulaya, Marekani na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.