Ghasia na machafuko yanaendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, suala ambalo limezidisha maafa na matatizo kwa raia wa kawaida hasa wanawake na watoto wadogo.

Melissa Hamuli mwenye umri wa miaka 30 anahangaika kuhama, maisha yake yamevurugika milele baada ya kutokea mapigano katika mji wa Mubambiro wa Kivu Kaskazini mapema mwaka huu. Ingawa alifanikiwa kukwepa kwa urahisi kuuawa, lakini miguu yake imekuwa na kilema na haifanyi kazi tena ipasavyo.

Amenukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Vita si jambo zuri. Vinasababisha watu wengi kuwa walemavu, wengine kufa. Tunaomba vimalizike, viongozi wa nchi watuhurumie.”

Melissa ni mmoja wa wagonjwa wengi katika kituo cha matibabu ya mifupa cha Shiŕika la Umoja wa Mataifa, mashariki mwa Kongo. Kituo hicho ambacho kinasaidiwa pia na Shirika la Kimataifa ya Msalaba Mwekundu tangu mwaka 2005, kwa muda mrefu kimekuwa kikitoa vifaa vya kuwasaidia kufanya kazi zao majeruhi wa vita. Lakini kadiri mapigano yanavyoongezeka ndivyo mahitaji nayo yanavyoongezeka.

Muhanga mwingine wa machafuko ya mashariki mwa DRC ni Amani Jérôme Jean-Claude, alipoteza mke na watoto wanne katika shambulio la makundi yenye silaha mwezi Aprili mwaka huu na yeye mwenyewe alijeruhiwa vibaya na kukatwa mguu.

Tangu mapema mwaka 2025, kituo hicho kimehudumia zaidi ya watu 800 waliojeruhiwa vibaya. Uzalishaji wa viungo bandia umeongezeka kutoka 422 mwaka mwaka mzima wa 2024 hadi 326 katika nusu ya kwanza tu ya 2025.

Watoto wasio na wazazi ni mgogoro mwingine mkubwa unaoitesa jamii ya Congo hasa maeneo ya mashariki, huku vitendo vya ubakaji, wizi na mauaji ya kiholela yakiripotiwa kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *