
Kaimu Waziri wa Polisi wa Afrika Kusini, Firoz Cachalia ametoa mwito kwa wananchi kulisaidia kikamilifu jeshi hilo katika kuweka ulinzi mkali wa kipolisi na uwekezaji wa kijamii ili kuzuia kuongezeka ghasia za magenge ya wahalifu kwenye Jimbo la Cape Magharibi.
Cachalia amesema hayo alipokuwa anahutubia kikao kidogo cha Bunge la Taifa na kuongeza kuwa: “Mgogoro wa ghasia za magenge ya wahalifu katika jimbo la ‘Rasi ya Magharibi …’ unasambaratisha jamii zetu, unakata maisha ya watu na unadhoofisha matumaini ya siku zijazo miongoni mwa watu wetu. Mgogoro huu unamhitaji kila mmoja wetu kuwa makini kikamilifu, kuoneshana huruma na kuchukua hatua za pamoja.”
Amebainisha kuwa, ghasia za magenge ya wahalifu katika jimbo hilo zimefikia viwango vya kutisha mwaka huu, huku watu wakiendelea kupigwa risasi na kuuawa au kujeruhiwa vibaya “kila siku.” Amesema, katika kipindi cha miezi sita iliyopita, kuanzia Aprili hadi Septemba, Jeshi la Polisi la Afrika Kusini limerekodi mauaji 490 yanayohusiana na magenge ya wahalifu.
Cachalia aidha amesema, magenge hayo yanazidi kuajiri vijana, akiongeza kuwa karibu vijana 120 walio na umri wa chini ya miaka 18 walipigwa risasi katika kipindi cha baina ya mwezi Aprili na Septemba mwaka huu, huku watoto wa chini ya miaka 14 wakisababisha vifo vya watu watano. Tangu mwezi Agosti, mauaji ya magenge ya wahalifu yameongezeka kwa asilimia 18 katika jimbo hilo la Rasi ya Magharibi (Western Cape) ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Cachalia amesema: Ni lazima tujiandae kutoa jibu kamili ambalo litatolwa na polisi kwa kushirikiana na raia wema katika kuzuia, kufungua mashtaka, kuhimiza uwekezaji wa kijamii na kuyakaribati upya maeneo yaliyoharibiwa na vitendo vya uhalifu.