
Serikali ya Sudan imewashutumu wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuwa wameshambulia kwa makusudi Msikiti mmoja huko El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini na kuua zaidi ya Waislamu 70 wakati wa Sala ya Alfajiri.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Jeneral al Burhan imelaani vikali shambulio hilo ililoliita ni “uvamizi mbaya wa kigaidi” dhidi ya Msikiti wa kitongoji cha Al-Daraja, ikisema kuwa, mashambulizi hayo yamejeruhi pia Waislamu kadhaa na kuharibu kwa kiasi fulani jengo hilo Msikiti.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shambulio hilo ni “ukiukaji wa wazi wa mafundisho ya kidini na mikataba ya kimataifa” inayolinda usalama wa raia na maeneo ya ibada.
Wizara hiyo imeilaumu RSF kwa kufanya unyanyasaji wa kimfumo dhidi ya raia na kuharibu miundombinu, na kuzitaka jumuiya za kimataifa kuchukua hatua dhidi ya “ugaidi unaowalenga raia wasio na silaha.”
Makundi ya kujitolea huko El Fasher yalisema mapema juzi Ijumaa kuwa zaidi ya watu 75 wameuawa, wakiwemo Wasudan 20 waliokimbia makazi yao na kukimbilia kambi ya Abu Shouk. Walisema ndege isiyo na rubani iliyokuwa ikiongozwa kwa mbali na kundi la RSF iligonga msikiti huo wakati wa Sala ya Alfajiri.
Mapigano kati ya RSF na Wanajeshi wa Sudan (SAF) na washirika wao yamepamba moto huko El Fasher tangu mwezi Mei mwaka huu.
Vita vya uchu wa madaraka kati ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF vilivyozuka mwezi Aprili 2023 huko Sudan, vimeshaua makumi ya maelfu watu na kuwalamisha mamilioni ya wengine kuhama makazi yao.