
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuchukua hatua kali ambazo hakuzitaja iwapo serikali ya Taliban nchini Afghanistan itakataa kukabidhi kituo cha jeshi la anga cha Bagram, ambacho kilitelekezwa wakati majeshi ya Marekani. yalipoondoka kifedheha katika ardhi ya nchi hiyo.
Wanajeshi wa Marekani walihama haraka katika kambi hiyo mnamo Julai 2021, mwezi mmoja kabla ya wapiganaji wa Taliban kuuteka mji mkuu Kabul, na kuiangusha serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na Washington na kukomesha ukaliaji wa mabavu wa Marekani wa ardhi ya nchi hiyo uliodumu kwa muda wa miaka 20.
“Ikiwa Afghanistan haitakirejesha kituo cha anga cha Bagram kwa wale walioijenga, yaani Marekani, MAMBO MABAYA YATATOKEA!!!”, ameandika Trump kwenye mtandao wa Truth Social, siku moja baada ya Afghanistan kumkatalia takwa lake hilo na kusisitiza kuwa Marekani haitaruhusiwa kuanzisha tena uwepo wake wa kijeshi katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.
“Afghanistan na Marekani zinahitaji kuzungumza… bila Marekani kudumisha uwepo wowote wa kijeshi katika sehemu yoyote ya Afghanistan,” alitamka bayana Zakir Jalal, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa serikali ya Taliban katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii.
Kituo cha jeshi la anga cha Bagram, asili yake kilijengwa na Umoja wa Kisovieti, na baadaye kikapanuliwa na kufanywa cha kisasa wakati Marekani ilipoivamia na kuikalia kijeshi Afghanistan, na kukitumia kama kituo chake kikubwa zaidi cha kijeshi nchini humo.
Trump ameshadai mara kadhaa kwamba China inakitumia kwa siri kituo hicho cha kijeshi, dai ambalo imekanushwa na Beijing na Taliban…/