Mkuu wa Majeshi ya kundi la Taliban nchini Afghanistan amesema: “Hatukubali mashinikizo ya Rais wa Marekani kuhusu kuutwaa tena Uwanja wa Ndege wa Bagram (ambao ulikuwa umegeuzwa kuwa kituo muhimu cha kikanda cha Washington kutokana na ukaribu wake na China).

Akijibu matamshi ya hivi karibuni ya Donald Trump kuhusu kurejea vikosi vya Marekani katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Bagram, Fasihuddin Fitrat, Mkuu wa Majeshi ya Kundi la Taliban, amesisitiza kwamba, Afghanistan leo hii ni nchi huru na kamwe haiko tayari kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo au kulazimishwa.

Fitrat, ambaye amesema hayo katika sherehe za kuhitimu Wanafunzi wa Jeshi la Anga la Wizara ya Ulinzi ya Taliban, amesisitiza kuwa, uhuru wa kisiasa na kijeshi wa Afghanistan ni kitu kisichojadilika na kuongeza kuwa: “Leo tena, Afghanistan si ya kikundi chochote cha kigeni na watu wetu hawatoruhusu nchi za kigeni kutuamulia nini cha kufanya.”

Akieleza kuwa jeshi la Taliban liko tayari kutetea mipaka yake na manufaa ya kitaifa, Fitrat amesema: “Taifa la Afghanistan limeonyesha katika historia kwamba linapinga aina yoyote ya uchokozi na kutenzwa nguvu. Hatushinikiziki wala hatuko tayari kujadiliana na wengine, maslahi ya taifa letu.”

Katika matamshi yake ya hivi karibu kabisa kwenye mtandao wa kijamii wa X-Net, rais wa Marekani Donald Trump alionya kwamba “mambo mabaya yatatokea ikiwa Afghanistan haitairejesha kambi ya jeshi la anga ya Bagram kwa wale walioijenga” akikusudia Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *