Mateka wa zamani wa Israel raia wa Marekani ambaye HAMAS ilimuonea huruma na kumwachilia huru, amethibitisha kivitendo kuwa “Fadhila za punda ni mateke.” Ametangaza kuwa anajiandaa kurejea Ghaza kwa sare za kijeshi za Israel kwenda kufanya mauaji zaidi ya kigaidi.

Edan Alexander, raia wa Marekani na Israel ambaye aliachiliwa huru kwa huruma ya HAMAS mwezi Mei mwaka huu, amejigamba kwamba kutumikia jeshi la utawala wa Kizayuni kufanya jinai ni moja ya heshima kubwa maishani mwake. 

“Mwezi ujao nitarudi Israel na kwa mara nyingine tena nitavaa sare yangu [ya jeshi la Israel], nikihudumu kwa fahari pamoja na ndugu zangu.” Alexander amesema hayo mjini New York, Marekani.

Lakini wakati huo huo Alexander ameitaka serikali ya Marekani kumshinikiza Benjamin Netanyahu kuanza tena mazungumzo ya mapatano ya kusitisha vita huko Ghaza na kuachiliwa huru mateka.

HAMAS ilimwachilia huru Alexander kama sehemu ya kuonesha nia njema na kwa ajili ya kufungua mlango wa mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru mateka, lakini leo hii Mmarekani huyo anasema yuko tayari kurejea Ghaza kwenda kufanya mauaji zaidi dhidi ya Wapalestina.

Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Ghaza tarehe 7 Oktoba, 2023, na hadi hivi sasa imeshaua kigaidi makumi ya maelfu ya Wapalestina wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

Huku hayo yakiripotiwa, familia za mateka wa utawala wa Kizayuni walioko mikononi mwa HAMAS zimeendelea kumlaani vikali waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kuwatelekeza jamaa zao na kukataa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *