
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali shambulizi la droni lililotokea hivi karibuni katika msikiti wa Al-Fashir, Sudan, ambalo limesababisha vifo na majeruhi kwa makumi ya waumini wa Kiislamu wasio na hatia.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, wizara hiyo imetaja shambulizi hilo kuwa “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu,” ikisisitiza umuhimu wa kusitishwa mara moja kwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu muhimu nchini Sudan.
Iran imetoa wito kwa pande zote husika kuendeleza mazungumzo ya “Wasudan kwa Wasudan” kama njia ya kumaliza mgogoro unaoendelea, huku ikieleza masikitiko na rambirambi kwa waathirika wa tukio hilo, na kuwatakia majeruhi uponyaji wa haraka na afya njema.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Sudan na waokoaji wa eneo hilo, zaidi ya watu 70 waliuawa Ijumaa baada ya waasi wa RSF kutekeleza shambulizi la droni dhidi ya msikiti huo.
Machafuko ya Ijumaa yanaashiria kuongezeka kwa mzozo wa miaka mitatu kati ya jeshi la Sudan na RSF, huku ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ikibainisha ongezeko kubwa la mashambulizi ya kikabila na vifo vya raia katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa kasi ya vifo vya raia imeongezeka kwa kiwango cha kutisha, watu 3,384 waliuawa ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, idadi inayowakilisha asilimia 80 ya vifo vyote vya raia vilivyoripotiwa mwaka mzima wa 2024.
Tangu Aprili 2023, vita vya Sudan vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu na kuwafanya takriban watu milioni 12 kukosa makazi. Umoja wa Mataifa umetaja mgogoro huo kuwa miongoni mwa majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku njaa ikizidi kuenea katika maeneo ya Darfur na kusini mwa Sudan.