Kambi ya Jeshi la Anga ya Bagram, ni moja ya vituo muhimu vya kijeshi nchini Afghanistan, na ni umuhimu hasa kutokana na kwamba ipo kwenye eneo la kimkakati, miundombinu yake ni ya hali ya juu, na inabeba jukumu muhimu katika masuala ya kijeshi, kisiasa na kijiografia.
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa ananuia kuiteka tena Kambi ya Anga ya Bagram nchini Afghanistan. Uamuzi huo wenye utata unatokana na mambo mengi yakiwemo malengo na shabaka za kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kijiografia. Lakini muhhimu zaidi ni kwamba kambi hiyo ya jeshi la anga iko kwenye eneo muhimu sana la kiistratijia.
Kambi ya Kijeshi ya Bagram iko umbali wa kilomita 40 kaskazini mwa Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. Ilijengwa na Wasovieti katika miaka ya 1950 na ilitumika kama kituo kikuu cha shughuli za kijeshi na vifaa vya Marekani na NATO nchini Afghanistan katika miaka 20 ya uvamizi wa Marekani na Wamagharibi yaani kuanzia mwaka 2001 hadi 2021. Ikiwa na barabara mbili ndefu za kurukia ndege, mabehewa makubwa ya ndege na vifaa vingi vya kilojistiki, kambi hiyo inahesabiwa kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya kijeshi nchini Afghanistan. Kambi hiyo ina uwezo mkubwa wa kupokea na kurusha droni na kusimamia kwa mbali utendaji kazi wa ndege hizo zisizo na rubani. Kambi hiyo iko karibu na mpaka wa Afghanistan na China, na suala hilo linaifanya Bagram kuwa na umuhimu usio na kifani kwa Marekani. Kituo hicho hakiko mbali sana na Iran na Russia lakini kiko karibu zaidi na China kwa umbali wa kilomita 92 tu. Trump anadai kuwa kutoka Bagram hadi kwenye vituo vya nyuklia vya China ni mwendo wa saa moja tu, hivyo lazima itekwe na ikaliwe tena kwa mabavu na Marekani.

Kwa kuongezea, huko nyuma kambi ya Bagram ilikuwa ikitumika kama kituo cha operesheni za kukabiliana na ugaidi dhidi ya vikundi kama vya al-Qaeda na ISIS. Miundombinu yake, ikiwa ni pamoja na hospitali ya vitanda 50 na gereza kubwa lenye ulinzi mkali, inasaidia kuendesha mambo kwa kina na umakini wa hali ya juu. Suhula za kambi hiyo pia zinawepesesha juhudi za kutafuta rasilimali tajiri ya madini huko Afghanistan kama vile madini ya lithiamu ambayo ni muhimu kwa mapinduzi ya teknolojia ya kisasa.
Kwa upande mwingine, moja ya mambo yanayomchochea Trump kung’angania kuiteka na kuikalia tena kwa mabavu kambi ya Bagram ni kuimarisha umaarufu wake wa kisiasa ndani ya Marekani. Kukimbia Marekani huko Afghanistan mwaka 2021 chini ya utawala wa Biden kumesbabisha ukosoaji mkubwa. Si tu kukimbia huko kulipelekea kuanguka serikali iliyokuwa inaungwa mkono na Marekani huko Afghanista, lakini pia kundi la Taliban lilichukua madaraka na kuhodhi kila kilichoachwa nyuma na Marekani vikiwemo vifaa vya mabilioni ya dola vya zana za kijeshi za Marekani huko Bagram na kwenye vituo vingine vya kijeshi nchini Afghanistan.
Trump, ambaye mara kwa mara alikuwa anaikosoa hatua ya Biden ya kukimbia Afghanistan na kuiita hatua hiyo kuwa maafa mabaya zaidi ya kijeshi ya Marekani, anajaribu kuhimiza kurejea kambi ya Bagram mikononi mwa Marekani na huo kwake ushindi wa kisiasa na ishara ya kurejesha mamlaka ya Marekani. Hatua hiyo inaweza kuvutia uungaji mkono kutoka kwa wahafidhina na wapiga kura wanaounga mkono wanamgambo wenye misimamo mikali nchini Marekani, hasa baada ya kumkosoa Biden wakati wa kampeni yake kwamba hakuwa na uwezo wa kusimamia namna ya kujiondoa Afghanistan.
Hivi sasa China imetanua uhusiano wake wa kiuchumi na Taliban tangu Marekani ilipokimbia Afgahnistan na Wachina wamewekeza katika miradi mikubwa ya madini na miundombinu nchini Afghanistan. Sasa kama Trump ataikalia tena kwa mabavu kambi ya Bagram huko Afghanistan, kutaiwezesha White House kufuatilia kwa karibu shughuli za China nchini Afghanistan.
Tab’an si jambo rahisi kwa Marekani kuikalia tena kwa mabavu kambi ya kijeshi ya Bagram kwani kundi la Taliban, ambalo linaiona Bagram kama ishara ya ushindi wake dhidi ya vikosi vya kigeni vinavyokalia kwa mabavu Afghanistan, inapinga vikali kurejea kijeshi Marekani nchini humo.
Tunaweza kusema kuwa iwapo Trump atashindwa kuiteka tena kambi ya kijeshi cha Bagram nchini Afghanistan atakuwa amezidi kujiharibia hasa kwa vile ahadi zake nyingi hajazitekeleza. Aliahidi kuziteka nchi za Canada na Greenland pamoja na Mfereji wa Panama lakini ameshindwa. Si rahisi kwa Marekani kuitwaa tena kambi ya Bagram isipokuwa kama Trump anataka kufanya makosa yale yale ya George W. Bush aliyeivamia Afghanistan mwaka 2001 lakini baadaye Marekani ikalazimika kukimbia kwa madhila nchini humo.