Jeshi la Niger limetangaza kuwa, Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya nchi hiyo vimeangamiza magaidi wasiopungua 34 wakati wa operesheni mbili zilizofanywa wiki iliyopita katika mikoa ya magharibi ya Dosso na Tillabery ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya kila wiki ya jeshi iliyotangazwa kwenye televisheni ya taifa, mapigano ya kwanza yalitokea siku ya Jumatano karibu na Doubalma katika eneo la Dosso, wakati doria kutoka Soukoukoutane iliposhambuliwa na magaidi wapatao 50 waliokuwa wamejihami kwa silaha wakiwa wamepanda pikipiki.

Jeshi la Niger limesema kuwa vikosi vyake, vikisaidiwa na jeshi la anga vilifanikiwa kuangamiza magaidi wasiopungua 22 na kujeruhi wengine wengi, huku washambuliaji waliosalia wakikimbia kuelekea ndani ya ardhi ya Mali.

Taarifa hiyo pia imesema: Wanajeshi saba wa Serikali waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Siku ya Ijumaa, operesheni nyingine ya ardhini ililenga genge la magaidi waliokuwa kwenye pikipiki wakisafirisha mifugo waliyoiiba karibu na Mangaize katika eneo la Tillabery.

Taarifa ya jeshi la Niger imesema:  Operesheni hiyo iliua magaidi wasiopungua 12, kuharibu pikipiki sita, na kuwezesha kupatikana mifugo yote iliyoibwa.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kutangaza kuwa, wanamgambo wenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh wameua zaidi ya raia 127 nchini Niger.

Shirika hilo liliripoti kwamba, hali ya kibinadamu ni mbaya sana katika maeneo ya ukanda wa Sahel ambayo mara kwa mara yamekuwa yakikumbwa na mashambulizi ya wanamgambo yakiwemo ya mkoa wa Tillaberi ulioko karibu na mpaka na Burkina Faso na Mali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *