
Jeshi la DRC limeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya waasi katika maeneo ya Masisi na Walikale katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki. Hayo ni kwa mujibu wa redio ya Umoja wa Mataifa Okapi.
Kwa mujibu wa redio hiyo, Jeshi la Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) siku ya Jumapili lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za waasi katika maeneo ya Masisi na Walikale, mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi.
Mashambulizi hayo yaliripotiwa katika vijiji vya Mukwengwa, Bibwe, Nyarushamba, Nyenge, na Hembe huko Masisi, na pia yalilenga ngome za waasi katika eneo la Peti, Walikale, kufuatia siku mbili za mapigano makali kati ya waasi na wanamgambo Wazalendo wanaounga mkono serikali.
Kwa mujibu wa redio ya Umoja wa Mataifa, vyanzo kadhaa vilithibitisha kuwa waasi walifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi katika vijiji vya Mukwengwa na Nyabikeri, ambapo watu kadhaa waliuawa na nyumba kuchomwa moto.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa.
Kurejea kwa kundi la waasi la M23 mwaka 2021 kulichochea zaidi mzozo huo. Kundi hilo linadhibiti maeneo makubwa, ikiwemo miji mikuu ya mkoa wa Goma na Bukavu, ambayo liiliteka mapema mwaka huu.
Mwezi Julai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na muungano wa makundi ya waasi, yakiwemo M23 (AFC/M23), walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano huko Doha yaliyopewa jina la Azimio la Kanuni.
Hata hivyo, mapigano mashariki mwa Kongo yanaendelea huku pande zote zikilaumiana kwa kuvunja mkataba wa kusitisha mapigano…/