Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusiana na mipango na malengo ya safari yake ya New York ya kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: “tutatangaza misimamo yetu kwa kuzingatia amani na usalama katika Umoja wa Mataifa.”

Leo asubuhi na baada ya kupiga kengele ya kuzindua kuanza mwaka mpya wa masomo nchini wa 1404-1405 kulingana na kalenda ya Iran ya hijria shamsia, na kabla ya kuondoka kuelekea New York kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Pezeshkian amesema kuhusu malengo ya safari yake hiyo: “safari yangu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni fursa nzuri ya kusikiliza hotuba za marais wa nchi na kubainisha misimamo yetu. Kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa mwaka huu ni “hali bora kwa sote” lakini msimamo wa kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na uimla ndio unaotawala kimataifa.

Rais wa Iran ameongezea kwa kusema: “baadhi ya nchi zinawaangamiza wanadamu wenzao kwa njia ya kikatili sana. Binadamu, akiwa ni mbora wa viumbe, anapaswa kuheshimiwa. Ni jambo la kutisha sana kuona watoto wakifa Ghaza kwa kukosa dawa na chakula. Israel inaripua Ghaza kila siku, na nchi ambazo eti zimestaarabika na zinadai kuwa ni watetezi wa demokrasia zinaiunga mkono na kuizatiti kwa silaha.”

Akizungumzia malengo yake katika safari yake ya New York, Pezeshkian amesema: “katika safari hii, nitatangaza misimamo yangu kwa kuzingatia imani niliyonayo kuhusu amani, uadilifu, ukweli na ubinadamu; na kama mazingira yataruhusu, nitafanya mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali, na pia Wairani na wataalamu walioko huko”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *