Viongozi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika AU na Umoja wa Ulaya EU, wametilia mkazo tena dhamira yao ya kuendeleza amani na maendeleo endelevu barani Afrika, kwa kuahidi ushirikiano wa kina zaidi ili kukomesha migogoro, kuimarisha mnepo na kukabiliana na changamoto za kimataifa kuanzia madeni hadi mabadiliko ya tabianchi.

Walipokutana katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kando ya wiki ya mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la umoja huo, viongozi wa taasisi hizo tatu wametoa tamko la pamoja baada ya mkutano wao wa pande tatu uliochukua muda wa masaa sita.

Wamesisitiza tena kuunga mkono mfumo wa kimataifa kama “njia bora zaidi ya kushughulikia changamoto za leo,” wakisisitiza utii kwa Hati ya Umoja wa Mataifa na kuonesha wasiwasi juu ya kuongezeka dharau dhidi ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu kote duniani.

Sehemu kubwa ya tamko hilo imejikita kwenye migogoro ya Afrika, hususan vita vinavyosababisha maafa makubwa nchini Sudan, ambavyo sasa viko katika mwaka wake wa tatu.

UN, AU na EU zimetoa wito wa kuongezwa msaada wa pamoja ili kuhakikisha “kusitishwa mapigano mara moja na kupatikana suluhisho endelevu” kupitia mazungumzo ya kisiasa jumuishi.

Kadhalika, viongozi wa taasisi hizo tatu muhimu kimataifa wamesema wataimarisha ushirikiano wa pande tatu ili kufanikisha suluhu zinazoongozwa na Waafrika wenyewe kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za amani na usalama.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya vilevile wameitaja Ajenda ya Afrika 2063 na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu kama mifumo ya mwongozo na wakazungumzia pia maandalizi ya Mkutano wa Kilele wa AU-EU utakaofanyika Angola mwezi Novemba mwaka huu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *