Mkutano Mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa umefunguliwa rasmi kwa hotuba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres. Katika hotuba yake hiyo Guterres amesema kuwa, hati ya Umoja wa Mataifa na sheria zake ziko chini ya mashinikizo na kusisitiza kwamba ni lazima tuchague kati ya ulimwengu uliojaa machafuko au ulimwengu uliojaa utulivu na amani.

Akiwa mtu wa kwanza kuhutubia kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema: “Nianze na maneno mawili ambayo hatujasema vya kutosha katika ukumbi huu. Kanuni za Umoja wa Mataifa ziko chini ya mashinikizo. Lazima tuchague kati ya ulimwengu uliojaa machafuko au ulimwengu uliojaa utulivu na amani.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia suala muhimu kimataifa na kutoa wito wa kusitishwa vita kwa sura ya kudumu huko Ghaza na kubadilishana mateka.

Amezungumzia pia jinsi Israel na Marekani zinavyowatesa kwa njaa watu wa Ghaza sambamba na mashambulizi yasiyokoma na kusema, inasikitisha kuona njaa inatumiwa kama silaha ya kuangamiza watu wasio na hatia. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amesema: “Watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari lazima walindwe, na uhuru wa kujieleza lazima uhifadhiwe. Suluhisho pekee linalofaa kwa amani ya Mashariki ya Kati ni suluhisho la serikali mbili.”

Viongozi wa dunia hukusanyika mjini New York kila Septemba kwa siku kadhaa za hotuba katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano huo unatoa fursa kwa viongozi wa mataifa ya dunia kupanda jukwaani na kuhutubia nchi wanachama kuelezea msimamo na maoni ya mataifa yao.

Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945 ukiwa na wanachama 51. Hivi sasa una wanachama 193. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *