Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kabla ya kuondoka kuelekea New York kwamba haiwezekani kuwa na mazungumzo na mtu yeyote ambaye ana nia ya “kulazimisha, kudhulumu, kufanya hila au kuvuruga mambo.”

Akizungumza Jumanne jijini Tehran kabla ya safari yake ya kuhutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Pezeshkian amesema mkutano huo ni fursa adhimu kwa viongozi wa dunia kutoa kauli zao na kwa Iran kuwasilisha misimamo yake.

Alieleza kuwa ingawa kaulimbiu ya mwaka huu ni “Muungano na Maendeleo,” hali halisi ya mambo duniani na mwenendo wa mataifa makubwa unaonyesha “ubinafsi na utawala wa mabavu.”

Rais Pezeshkian ameeleza kwa uchungu mkubwa hali ya watoto wanaofariki huko Gaza, akilaani mataifa yanayounga mkono na kusambaza silaha kwa Israel katika mashambulizi yake ya kila siku.

Ameashiria majibu ya jumuiya ya kimataifa kuhusu uhalifu huo na kuhoji hivi, je, “muungano” unamaanisha kwamba watu wote wauawe ili kutii mamlaka ya nguvu moja? Rais wa Iran amesisitiza kuwa binadamu wote wana haki ya “kufaidika na neema zote alizotoa Mwenyezi Mungu.”

Rais Pezeshkian ameelezea malengo ya ziara yake, akisema atatangaza misimamo yake kwa msingi wa imani katika “amani, haki, haki za binadamu, na utu.”

Ameongeza kuwa atafanya mazungumzo na viongozi wa mataifa mbalimbali iwapo hali itaruhusu, na pia atakutana na Wairani na wataalamu walioko nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa mataifa “yanapaswa kuketi pamoja na kuzungumza ili kuelewana,” lakini haiwezekani kuzungumza na mtu “anayelazimisha, kudhulumu, kufanya hila au kuharibu.”

Ameongeza kuwa: “Si sahihi kwamba Israel tu ndiyo ipate usalama; usalama wa watu wote duniani lazima ulindwe.”  Rais wa Iran ameahidi kutumia “fursa ya kipekee” ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha misimamo ya Iran “inasikika kwa uwazi duniani huko New York.”

Viongozi wa dunia wanakusanyika New York kuhutubia Mkutano Mkuu wa kila mwaka kuanzia Septemba 23 hadi 29.

Kaulimbiu ya mjadala wa mwaka huu, “Bora kwa pamoja: Miaka 80 na zaidi kwa amani, maendeleo na haki za binadamu,” inaadhimisha miaka ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa na inasisitiza wito wa kujitolea upya kwa mshikamano wa kimataifa, ushirikiano, na hatua za pamoja kwa ajili ya watu na sayari.

Katika chapisho la X siku ya Jumapili, mshauri wa kisiasa wa rais wa Iran, Mehdi Sanaei, alisema Pezeshkian anatarajiwa kutoa hotuba yake katika Mkutano Mkuu wa UN siku ya Jumatano asubuhi kwa saa za huko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *