Waziri Mkuu wa India amewataka wananchi wa nchi hiyo kuacha kutumia bidhaa kutoka nje na badala yake watumie bidhaa za ndani kufuatia kushtadi mivutano katika uhusiano wa nchi hiyo na Marekani.
Baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuweka ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa kutoka India, Narendra Modi Waziri Mkuu, amewatolea wito wananchi wa nchi hiyo kutumia bidhaa za ndani zinazolishwa nchini. Modi Siku ya Jumapili alisema katika hotuba kwa taifa kabla ya kutekeleza mpango mkubwa wa kupunguza ushuru kwa bidhaa mbalimbali za mahitajio kwamba: Bidhaa nyingi tunazotumia kila siku zinatengenezwa nje ya nchi, lakini hatuzifahamu. Tunapaswa kuachana na bidhaa hizi. Modi bila ya kutaja nchi, alisema “tunapasa kununua bidhaa zinazotengenezwa India.” Aidha aliwataka wamiliki wa maduka kuzingatia uuzaji wa bidhaa zinazotengenezwa India, akisema kuwa hii itazidisha ukuaji wa uchumi wa nchi. Katika wiki za karibuni makampuni mengi ya India yamezidisha kampeni za kutangaza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini humo.
Wafuasi wa Waziri Mkuu wa India wameanzisha kampeni za kususia makampuni ya Kimarekani yakiwemo makampuni ya McDonald’s, Pepsi na Apple ambayo ni mashuhuri sana huko India. Jamii ya watu bilioni 1.4 wa India ni soko kubwa la bidhaa mbalimbali za mahitaji kutoka Marekani ambazo aghalabu hununuliwa kutoka duka la kidijitali la Amazon nchini humo.
Uhusiano wa India na Marekani umekumbwa na mvutano tangu mwezi Juni mwaka huu. Hitilafu za awali za kidiplomasia zilichochewa na matamshi makali ya Washington dhidi ya New Delhi na hatua ya Marekani ya kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za India; hata hivyo India imejaribu kuepuka kuingizwa katika makabiliano ya moja kwa moja na Marekani na kudumisha kujitawala kwake kimkakati. Waziri wa Biashara wa India Poojay Goyal anatazamia kuitembelea Washington hivi karibuni ili kujaribu kufikia makubaliano katika mazungumzo ya biashara na Marekani. Ziara hii tarajiwa itafanyika katika kalibu ya juhudi za kupunguza mivutano katika uhusiano kati ya pande mbili.
Pamoja na kuwa wito uliotolewa na Narendra Modi katika hotuba yake ya karibuni haukuitaja wazi Marekani, lakini tamko lake la kutilia mkazo kutumiwa pakubwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya India limefungamanishwa na kuongezeka mivutano kati ya nchi hiyo na Marekani hasa baada ya Rais Donald Trump kutangaza kuziwekea ushuru wa asilimia 50 bidhaa za India zinazoingizwa Marekani. Mivutano na sera hizi zinaweza kuonekana kama motisha kwa India ili kuimarisha uwezo wa kujitosheleza kwa bidhaa na kupunguza kutegemea masoko ya nje, hasa soko la Marekani. Aidha kuna nukta muhimu kadhaa katika uwanja huo.

Mosi: Athari za ushuru kwa mauzo ya nje: Akiwa katika muhula wa pili wa urais Donald Trump ametangaza ushuru wa kiwango cha juu kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka India. Sera hizi zimetoa mashinikizo kwa bidhaa zinazoingia Marekani kutoka India na wakati huo huo kupunguza ushindani kwa bidhaa za India katika soko la Marekani. India sasa inafanya kila iwezalo ili kuimarisha uzalishaji wake wa ndani na kupunguza kutegemea masoko ya nje ili kukabiliana na hali hii na hivyo kuzuia kuathiriwa na sera kama hizi katika siku zijazo.
Pili: Utegemezi wa kiwango cha chini kwa Marekani: Baada ya Marekani kushadidisha tozo zake za ushuru na kuweka vizuizi mbalimbali vya kibiashara, India imeamua kujikita katika kuboresha uzalishaji wa ndani wa bidhaa mbalimbali za mahitaji ya muhimu na kujielekeza katika masoko mengine ili kulinda ukuaji wake wa kiuchumi. Hatua hii inaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa India kwa Marekani na kwa nchi nyingine na kukabiliana pakubwa na mashinikizo ya kiuchumi na kibiashara.
Tatu: Kupiga hatua kuelekea kujitosheleza: Sera ya “Atma Nirbar Bharat” (India inayojitegemea) ambayo Modi anaifuatilia pakubwa ni jibu kwa changamoto kama vile ushuru na ukwamishaji wa kibiashara. Lengo la sera hii ni kuimarisha viwanda vya ndani na kupunguza kutegemea bidhaa kutoka nje.
Nne: Kupunguza taathira za kiuchumi: Kwa kuzingatia kuwa, ushuru na mivutano ya kibiashara inaweza kuwa na taathira hasi kwa uchumi wa India, serikali ya Modi kwa upande wake inafanya kila linalowezekana ili kuilinda India kufuatia kubadilika uchumi wa dunia na sera za kibiashara za Marekani kwa kuimarisha uzalishaji wa viwanda vya ndani, kuandaa fursa za ajira na kupunguza kutegemea masoko ya nje.
Kiujumla, wito wa Modi wa kusisitiza kutumiwa bidhaa za ndani ni jibu kwa changamoto za kibiashara na mashinikizo ya kiuchumi ambayo ni natija ya sera za Marekani, hasa ushuru uliotangazwa na Marekani kwa bidhaa za India. Hatua hii itasaidia India kukabiliana pakubwa na matukio ya kiuchumi na mivutano ya kibiashara duniani.