
Ndege iliyokuwa imembeba waziri mkuu wa Israel ambaye ni maarufu kwa jina la nduli wa Ghaza na ambaye anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kujibu mashtaka ya jinai za kivita anazofanya huko Ghaza, imelazimika kuruka masafa marefu kukwepa anga za nchi kadhaa za Ulaya alipokuwa anaelekea Marekani.
Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kunukuu taarifa ya shirika la redio na televisheni la Israel ikithibitisha kwamba, ndege ya Netanyahu ilikwepa kuruka katika anga za nchi za Ulaya isipokuwa Ugiriki na Italia wakati wa safari yake ya kuelekea Marekani. Masafa hayo mapya yaliyokatwa na ndege ya Netanyahu yameongeza takriban kilomita 600 zaidi.
Licha ya kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya binadamu, lakini Netanyahu mwenyewe ni mwoga mno wa kufa. Sababu ya kulazimika ndege yake kuruka masafa marefu ni woga na kihoro chake cha kukamatwa na kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Netanyahu amelazimika kukwepa kuruka kwenye anga za nchi ambazo zinaweza kutekeleza amri ya kumtia mbaroni na kumburuza mahakama The Hague kwenda kujibu mashtaka yasiyo na idadi ya jinai za kivita na ukatili dhidi ya ubinadamu anaowafanyia wananchi wa Palestina hasa wa Ghaza.
Huko nyuma pia na katika safari kadhaa zilizopita, muda wote hofu na kihoro cha kutiwa mbaroni kinamwandama Netanyahu na ndio maana analazimisha ndege ya zinazomchukua kuruka masafa marefu zaidi.
Mwezi Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ilitoa hati ya kukamatwa Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za jinai za kutisha za kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Ghaza. Wahanga wakubwa wa jinai za Netanyahu ni wanawake, watoto wadogo na vizee wasio na ulinzi.