
Kamanda mwandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, utawala wa kizayuni wa Israel hauna uwezo wa kupigana bila ya kusaidiwa na shirika la kijeshi la NATO na Marekani, jambo linalodhihirisha kuwa makabiliano yanayoweza kutokea ni ya mpambano dhidi ya “ubeberu wa kimataifa.”
Admeri Habibollah Sayyari, Naibu Mkuu wa Jeshi la Iran ameyasema hayo katika mahojiano kwa mnasaba wa Wiki ya Kujihami Kutakatifu ya kuadhimisha miaka minane ya vita vya kichokozi vilivyoanzishwa dhidi ya Iran na dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein katika miaka ya 1980.
Akiashiria vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran katika miaka ya 1980 na uvamizi wa Marekani na Israel mnamo mwezi Juni, Admeri Sayyari amesema lengo la adui katika vita vyote viwili lilikuwa “kuyashinda Mapinduzi [ya Kiislamu] na kuulenga umoja wa ardhi yote ya nchi”.
Kamanda mwandamizi wa Iran amebainisha kuwa utawala wa kizayuni wa Israel hauna uwezo wa kupigana bila ya kusaidiwa na NATO na Marekani, na akaongeza kwamba, wakati wa vita vya siku 12, Iran ilitoa “vipigo vikali” kwa utawala huo ambao ulichujwa usionekane mbele ya macho ya walimwengu, na hatimaye ukabaki “umepondwa pondwa,” kwa alivyoelezwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Admeri Sayyari amebainisha kuwa, katika vita vyote viwili, “adui alikuja kwenye medani na vikosi vyake vya niaba, mara moja akimtumia Saddam na mara nyingine akiutumia utawala wa Kizayuni.”
Kwa mujibu wa kamanda huyo, katika vita vyote viwili, waliwaandalia wavamizi “zana zote zilizohitajika; wakati ule, Mashariki na Magharibi zilikuwa nyuma ya Saddam, na leo, NATO na ubeberu wa kimataifa ziko upande wa Netanyahu.”
“Mifanano hii inaonyesha kwamba hata hii leo, ubeberu wa kimataifa umesimama mbele yetu. Ni fahari kwetu kwamba ikiwa tunapigana, tunapigana dhidi ya ubeberu, si dhidi ya maadui wadogowadogo,” amesisitiza kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la Iran…/