Vita vya Ukraine, vilivyoanza mwishoni mwa mwezi Februari 2022, vimeleta mabadiliko makubwa ya kijiografia na kisiasa ulimwenguni.
Kwa mujibu wa Pars Today, vita hivyo havijasababisha tu athari kubwa za kisiasa, kiuchumi na kijamii, bali pia vimeongeza mahitaji ya silaha na zana za kijeshi duniani. Hali hiyo imeyapa mashirika ya silaha ya Marekani utajiri usioelezeka bila ya kujali damu za watu zinazomwagika. Hapa tutaangalia kwa muhtasari jinsi mashirika ya silaha ya Marekani yanavyopata faida kubwa sana kutokana na vita vya Ukraine.
Mosi – Matokeo makuu ya vita vya Ukraine ni ongezeko kubwa la mahitaji ya silaha za kisasa duniani. Nchi za Magharibi, hasa Marekani, zimeendelea kumimina misaada ya kijeshi nchini Ukraine kujaribishia silaha zake. Misaada hiyo inajumuisha aina mbalimbali za silaha, zikiwemo ndege, makombora, vifaru, magari ya deraya, mifumo ya ulinzi wa anga, silaha nyepesi na “nusu nyepesi,” na kadhalika. Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa la mapato ya makampuni ya silaha ya Marekani kupitia damu za watu zinazomwagwa kila leo. Mashirika kama Lockheed Martin, Raytheon, Boeing, General Dynamics na Northrop Grumman ndio watengenezaji wakubwa zaidi wa silaha nchini Marekani ambao wametumia fursa hiyo vizuri sana. Hasa kwa kuzingatia kuwa kandarasi ambazo mashirika hayo yamepewa na serikali ya Marekani zinayawezesha kuendesha miradi mingi ya silaha na kujiingizia faida kubwa kupindukia.

Pili – Vilevile Marekani imetuma takriban dola bilioni 160 za msaada wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine tangu kuanza vita kati yake na Russia. Msaada huo unajumuisha silaha za kisasa, mafunzo na vifaa vya huduma za raia ambavyo vingi vinazalishwa nchini Marekani. Sera hiyo imekuwa ya manufaa kwa makampuni ya silaha ya Marekani na madhara makubwa kwa raia wa Ukraine.
Kwa mfano, shirika la Raytheon, mtengenezaji mkuu wa mifumo ya ulinzi wa anga kama vile mfumo wa makombora wa Patriot, limeweza kupata kandarasi mpya ya serikali ya Marekani ya kusambaza mifumo hiyo nchini Ukraine. Shirika la Lockheed Martin, mtengenezaji wa makombora ya kukabiliana na vifaru yaitwayo Javelin na mifumo ya maroketi ya HIMARS, pia limenufaika mno na vita vya Ukraine. Makampuni haya yanafaidika si tu kutokana na mauzo ya silaha kwa Ukraine, lakini pia kutokana na mauzo ya silaha kwa washirika wengine wa Marekani ambao wanaimarisha uwezo wao wa ulinzi. Nchi kama Ujerumani, Poland, Romania na nchi za Skandinavia kama Norway na Denmark, pamoja na Uholanzi, zimekuwa zikinunua silaha za Marekani kwa kasi, zikidai kuwa Russia inatishia usalama wao.
Tatu – Ingawa faida za makampuni ya silaha ya Marekani kutokana na vita vya Ukraine zinahusiana moja kwa moja na uuzaji wa silaha na vifaa vinginevyo, lakini athari zake za muda mrefu kwenye soko la hisa pia ni muhimu. Tangu mwanzo wa vita, hisa za mashirika ya silaha ya Marekani zimeongezeka kwa kasi. Kwa mfano, hisa za Lockheed Martin zimeongezeka kwa takriban 30% tangu mwezi Februari 2022. Ongezeko hili limetokana na matarajio ya mauzo ya silaha na kuongezeka mahitaji ya silaha ya madola ya Magharibi yanayodai kuwa yanaogopa kushambuliwa na Russia. Mashirika mengine pia yamepata ustawi kama huo kutokana na vita vya Ukraine. Shirika la Northrop Grumman, moja ya watengenezaji wa mifumo ya kisasa ulinzi, limeongeza mapato yake kutokana na kuongezeka mahitaji ya zana za kivita na kutokana na maombi mengi kutoka kwa washirika wa Marekani.

Nne – Sababu nyingine ambayo imechangia kupata faida nono mashirika ya silaha ya Marekani kutokana na vita vya Ukraine ni nguvu ya lobi za viwanda vya silaha nchini Marekani. Ushawishi wa mashirika hayo una nafasi kuu katika kuunda sera ya ulinzi ya Marekani. Mashirika hayo yana ushawishi mkubwa ndani ya serikali za Marekani kwenye nyuga zote. Kwa mfano, taasisi vile AIPAC ambayo ni muungaji mkono mkuu wa jinai za Israel, mara nyingi zinaunga mkono uuzaji wa silaha za Marekani kwa nchi maalumu kama vile Ukraine.
Hata hivyo na ingawa faida za mashirika ya silaha ya Marekani ni kubwa kutokana na vita vya Ukraine, lakini suala hilo lina changamoto nyingi. Hivi sasa kuna wasiwasi kuhusu athari mbaya kwenye siasa na usalama wa kimataifa. Wakosoaji wanaamini kwamba faida za mashirika hayo ya silaha ya Marekani huenda zikazichochea serikali za Washington kuzusha vita na migogoro zaidi kwenye kona tovauti duniani ili kulinda maslahi hayo haramu. Kwa kuongezea ni kwamba, kuna wasiwasi wa kurefuka vita na athari zake za kibinadamu. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, makampuni ya silaha ya Marekani yana uwezekano mkubwa wa kuuza silaha zao na kuendesha vita vya muda mrefu ili kujiongezea mapato.