Rwanda imetangaza kuwa, jana Jumatano ilipokea wakimbizi 314 raia wa nchi hiyo waliorejeshwa Rwanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Wizara ya Usimamizi wa Masuala ya Dharura ya Rwanda imesema katika taarifa hiyo kwamba waliorudishwa ni pamoja na familia 101 za Wanyarwanda na watahifadhiwa kwa muda katika Kituo cha Nyarushishi katika wilaya ya magharibi mwa nchi hiyo ya Rusizi ili kutoa nafasi ya kufanyika taratibu za usajili na kuwarejesha nyumbani, ikiwa ni pamoja na mipango ya kuhakikisha wanarejeshwa kwenye maeneo yao kwa usalama na heshima.

Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Rwanda imeanzisha mipango ya kuwaingiza pia watu wengine kwenye mpango huo ili kuwasaidia kupata makazi endelevu na ya kudumu watu wanaorejea nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuwa elimu watoto wao, huduma za afya n.k.

Wizara hiyo ilisisitiza dhamira ya serikali ya Kigali ya kuunga mkono zoezi la kurejeshwa nyumbani wakimbizi wa Rwanda kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Naye Meya wa Wilaya ya Rubavu, Prosper Mulindwa, amewataka wanaorejea nchini Rwanda kushiriki katika miradi ya maendeleo kwenye jamii zao ili kupambana na umaskini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Usimamizi wa Masuala ya Dharura ya Rwanda,  zaidi ya Wanyarwanda 4,000 wamerejea nchini humo kutoka DRC tangu mwezi Januari mwaka huu.

Mwezi Julai, Rwanda, DRC na UNHCR zilitia saini makubaliano ya kuheshimiwa haki ya wakimbiziya  kurejea katika nchi zao za asili kwa hiari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *