Serikali nchini Madagascar imetangaza marufuku ya kutoka nje usiku kufuatia maandamano yaliyoshuhudia polisi wakitumia risasi za mpira na gesi ya kutowa machozi kutawanya waandamanaji wanaolalamikia mgao wa umeme na maji.

Mamia ya waandamanaji waliingia mitaani kupinga mgao wa mara kwa mara wa umeme ambao unakatika kwa zaidi ya saa 12. Waandamanaji walizuia barabara kwa kutumia matairi na mawe. Kumekuwa na ripoti za uporaji wa maduka na benki katika mji mkuu wa taifa hilo la kisiwa cha Bahari ya Hindi.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo pia vimeripoti kwamba nyumba za wanasiasa watatu walio karibu na Rais Andry Nirina Rajoelina zilivamiwa na waandamanaji. Vuguvugu la maandamano, lililotawaliwa zaidi na vijana, lilianza kupata mvuto siku chache zilizopita kwenye mitandao ya kijamii, haswa Facebook.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *