
Barua ya siri iliyoonekana na shirika la habari la Associated Press, imeelezea kusitishwa kwa ushirikiano huo katika wakati ambapo kuna mvutano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Barua hiyo ya Septemba 17 kutoka wizara ya mambo ya nje ya Mali kwa ubalozi wa Ufaransa mjini Bamako, imesema wafanyakazi hao watano wametangazwa kuwa “watu wasiokaribishwa” na ikatangaza pia kusitishwa kwa ushirikiano wote wa kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Hata hivyo, barua hiyo ya wizara haikutoa sababu ya kufukuzwa kwa wafanyakazi hao.
Chanzo cha kidiplomasia cha Ufaransa kimeiambia AP kwamba hatua hiyo ya Mali ilikuwa jibu kwa uamuzi ya Ufaransa wiki iliyopita wa kuwafukuza maafisa wawili wa kijasusi wa Mali waliokuwa wakifanya kazi katika ubalozi wa Mali mjini Paris .