Colombia imetoa wito wa kuundwa jeshi la kimataifa la kukabiliana na utawala wa kizayuni wa Israel.

Wito huo umetolewa na Rais wa nchi hiyo Gustavo Petro, katika hotuba yake aliyotoa siku ya Jumanne kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo alizitaka nchi za Upande wa Kusini mwa Dunia (Global South) ziunde jeshi la kimataifa ili “kuikomboa Palestina” na kukabiliana na “dhulma na ukandamizaji” unaoungwa mkono na Marekani na NATO.

Rais wa Colombia alizitaka nchi hizo zijiandae kuunda jeshi imara la kuwalinda watu wa Palestina na “kutetea ubinadamu.” Petro alisisitiza katika hotuba yake hiyo kwamba nchi ambazo “haziyakubali mauaji ya halaiki” lazima ziunde “kikosi chenye silaha cha kulinda maisha ya watu wa Palestina.”

Rais wa Colombia aliwahutubu hadhirina akisema: “tunahitaji jeshi imara kutoka nchi ambazo haziyakubali mauaji ya halaiki. Kwa sababu hii, ninatoa wito kwa mataifa na nchi za ulimwengu, zichukue, zaidi ya chochote kile, hatua ya kukusanya silaha na vikosi vya kijeshi, ikiwa ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na ubinadamu. Lazima tuikomboe Palestina”.

Petro ameongezea kueleza kwamba, Washington na NATO sasa hivi “zinaua demokrasia” na kufufua “uimla na ukritimba” katika upeo wa kimataifa, na akazungumzia udharura wa kuinua “bendera ya uhuru au kifo,” ambayo kwa kauli yake yeye inapasa iambatane na rangi nyeupe ya amani na matumaini. Kufuatia matamshi aliyotoa rais wa Colombia na ukosoaji wake kwa rais wa Marekani, ujumbe wa Marekani uliondoka kwenye kikao hicho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hatua iliyooonekana kuwa ni ishara ya malalamiko ya Washington.

Bendera ya Palestina

Katika miezi ya karibuni, Colombia ikiwa ni nchi moja ya Amerika ya Kusini, imechukua hatua kubwa kuunga mkono kadhia ya Palestina, kuanzia kuvunja uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia mpaka kuisusia Israel. Moja ya mabadiliko muhimu yaliyojiri katika uga huo ni wito huo uliotolewa na viongozi wa Colombia wa kuunda “jeshi imara” kwa ajili ya kuikomboa Palestina. Kuhusiana na suala hili, kuna sababu kadhaa tunazoweza kuziashiria hapa:

Ya kwanza ni ya chimbuko la kihistoria na kisiasa: Colombia daima imekuwa ikikabiliwa na masuala tata ya ndani na nje katika historia yake yote. Nchi hiyo ilikumbwa na vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimesababisha mabadiliko makubwa katika sera zake za nje. Katika miaka ya hivi karibuni, Bogota imejaribu kuanzisha uhusiano wa karibu na nchi mbalimbali, zikiwemo za Asia Magharibi. Colombia imekuwa mara nyingi ikiyapa umuhimu masuala ya kimataifa na ya kibinadamu, kwa kuunga mkono haki za binadamu na kupiga vita dhulma duniani. Suala la Palestina ambalo katika maeneo mengi ulimwenguni linachukuliwa kuwa ni kadhia ya kiutu na kisiasa nalo pia lina umuhimu mkubwa kwa Colombia.

Nukta ya pili inahusiana na sababu za kisiasa: Wito wa Colombia wa kuundwa jeshi imara la kuikomboa Palestina linatokana na sababu kadhaa za kisiasa. Kwanza ni kwamba, hatua hii inaweza kusaidia kuimarisha uhusiano wa Colombia na nchi za Kiarabu, hususan zile zinazoiunga mkono Palestina. Colombia inapigania kuwa na nafasi ya juu kwenye uga wa kimataifa katika sera zake za nje, na kwa kufanya hivyo, kujitambulisha kama nchi inayounga mkono haki za binadamu na uadilifu kimataifa. Lakini pili ni kuwa, wito huo iliotoa unaweza ukawa ni mjibizo kwa sera za Israel na Marekani kuhusiana na Palestina. Colombia imezidi kukosoa mitazamo ya nchi za Magharibi katika masuala ya kimataifa, ikiwemo Palestina, hasa baada ya mabadiliko ya kisiasa yaliyojiri nchini humo katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuingia madarakani rais wake mpya Gustavo Petro.

Ama kuhusiana na mijibizo na changamoto, wito wa Colombia wa kuundwa jeshi imara la kuikomboa Palestina limepokewa kwa hisia na maoni tofauti. Baadhi ya wachambuzi wanauchukulia wito huo kama harakati ya kialama tu inayolenga kuvutia hisia na kutoa mguso kwa kadhia ya Palestina. Katika upande mwingine, baadhi ya nchi za Magharibi hususan Marekani haijafurahishwa na hatua hiyo, jambo ambalo lilidhihirishwa na ujumbe wa nchi hiyo kwa kutoka nje ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya Rais wa Colombia uundaji wa jeshi la kimataifa la kukabiliana na utawala wa kizayuni wa Israel. Lisilo na chembe ya shaka ni kuwa msimamo wa aina yake alioonyesha Gustavo Petro juu ya suala hilo utaathiri uhusiano wa Colombia na nchi za Magharibi hasa Marekani. Kwa upande mwingine, kuunda jeshi imara la kuikomboa Palestina kunaweza kukabiliwa na changamoto kubwa za kijeshi na kiuchumi. Colombia inahitaji mtaji mkubwa wa kifedha na kijeshi ili kufanikisha lengo hilo, jambo ambalo liko nje ya uwezo wake; na ni wazi kwamba, kupatikana kwa kikosi hicho cha kimataifa kutahitaji ushirikiano ulioratibiwa wa nchi mbalimbali duniani.

Hitimisho la yote haya ni kuwa, wito wa Colombia wa kuundwa jeshi imara la kuikomboa Palestina unaashiria mabadiliko mapya katika sera za nje za nchi hiyo. Hatua hiyo kwa sehemu kubwa inaonekana kama ya kialama katika kuunga mkono haki za Wapalestina na kutoa mguso wa mazingatio kwa kadhia ya Palestina. Pamoja na hayo, ufuatiliaji wa lengo hilo utakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zitakuwa na athari kubwa na za muda mrefu kwa sera za ndani na nje za Colombia…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *