
Mchakato wa zoezi la uchaguzi wa bunge jipya nchini Syria sio mchakato rahisi na kuna maswala kadhaa ambayo yanaleta mkanganyiko. Kwanza ifahamike kwamba mchakato wa uchaguzi wa bunge ni mchakato mpana, sio kila raia atakwenda kupiga kura na wala hakutakuwa na vyama vya kisiasa au mabango ya kampeini.
Badala yake kura zitapigwa na kamati mbali mbali zilizoundwa na hii ndiyo sababu uchaguzi huu wa kwanza kufanyika baada ya utawala wa kidikteta unatajwa kama uchaguzi usiokuwa wa moja kwa moja.
Serikali ya mpito ya Syria ilishatoa ufafanuzi mnamo mwishoni mwa mwezi Juni,kwanini uchaguzi hautowashirikisha moja kwa moja raia kupiga kura. Serikali hiyo ilisema uhalisia uliopo sasa nchini humo hauruhusu uchaguzi kufanyika kama ilivyozoeleka kutokana na kutokuwepo kwa mamilioni ya watu wanaoishi nje ya Syriana walioachwa bila makaazi ndani ya Syria.
Kukosekana kwa vibali rasmi na mfumo dhaifu wa kisheria ni baadhi ya sababu nyingine zilizotajwa.
Kutokana na yote hayo mchakato wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo wa bunge utakaofanyika tarehe 5 Oktoba, utaendeshwa kwa awamu kadhaa. Mnamo mwezi Juni serikali ya mpito iliteuwa moja kwa moja kamati kuu ya uchaguzi huo inayojumuisha watu 11.
Orodha ya mwisho ya wagombea ilishatangazwa tangu Septemba 18
Kamati hiyo baadae iliteuwa kile kinachojulikana kama kamati ndugo za uchaguzi katika wilaya 62 za uchaguzi nchini Syria. Na wilaya hizo zimeundwa kwa kuzingatia idadi ya wakaazi wake ambapo baadhi ya wilaya hizo zitakuwa na haki ya kuchagua zaidi ya mbunge mmoja.
Hatua ya pili itakayofuatia ni kwamba kamati hizo ndogo za uchaguzi zitatakiwa kuteua kati ya wawakilishi 30 na 50 watakaochukuwa viti vya uwakilishi kwenye wilaya zao na kisha wawakilishi hao wataunda kile kinachoitwa kamati kuu ya uchaguzi ambayo ni kundi la wapiga kura lililopewa jukumu la kuwachagua wabunge.
Kamati hizo ndogo zitatakiwa kuzingatia mambo kadhaa kabla ya kuwachagua wabunge hao, na miongoni mwa vigezo wanavyotakiwa kuzingatia ni pamoja na elimu na taaluma za watakaowachagua,ushawishi wao katika jamii miongoni mwa mengine lakini pia wanatakiwa kuhakikisha kwamba watakaowachagua wanajumuisha makundi ya watu walioachwa bila makaazi, walemavu na waliowahi kufungwa jela.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari nchini Syria-SANAorodha ya mwisho ya wagombea ilishatangazwa tangu Septemba 18 na wananchi hivi sasa wana muda wa siku tatu kukata rufaa dhidi ya mgombea yoyote wanayemuona hafai kuwa kwenye orodha hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari nchini Syria zinaonesha kwamba wengi wa raia nchini humo wanakubaliana kwamba hakuna uwezekano wa kufanyika uchaguzi utakaowahusisha moja kwa moja raia kwa hivi sasa.