Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Slovenia, nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya “haitamruhusu Netanyahu kuingia kwenye ardhi” yake, ikisema inataka kulinda heshima ya sheria za kimataifa

Tangazo hilo linalohusishwa na waranti wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa dhidi ya Netanyahu na wenzake, limekuja wakati tayari Slovenia imeshawapiga marufuku mawaziri wengine wawili wa serikali ya Netanyahu, Itamar Ben-Gvir anayehusika na usalama wa taifa, na Bezalel Smotrich anayehusika na masuala ya fedha.

Msemaji wa wizara ya nje ya Slovenia, Neva Grasic, alisema mataifa yote “yaliyosaini mkataba wa mahakama hiyo ya kimataifa yana wajibu wa kutotambua ukaliaji kimabavu wa Israel dhidi ya ardhi ya Palestina na hayatakiwi kuipa msaada wowote unaoiwezesha kuendelea na ukaliaji huo.” 

Slovenia pia ilishatangaza marufuku ya silaha dhidi ya Israel, kutokana na kile kinachoendelea kwenye  Ukanda wa Gaza

Italia, Uhispania zatuma meli za kijeshi kulinda msafara wa misaada

Uhispania  na Italia zilisema zimetuma meli za kijeshi kuusindikiza msafara wa misaada ya kibinaadamu unaoelekea Gaza, baada ya waandaaji wa msafara huo kusema wameshambuliwa kwa droni wakiwa kwenye bahari ya Ugiriki. 

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.
Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.Picha: Toby Melville/AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, alisema siku ya Alkhamis (Septemba 25) kwamba serikali yake inataka kuona sheria za kimataifa zikiheshimiwa na haki ya raia wake kutumia Bahari ya Mediterania inalindwa ipasavyo. 

Waziri wa Ulinzi wa Italia, Guido Crosetto, aliliambia bunge mjini Roma kwamba serikal yake inalaani vikali mashambulizi hayo ya droni, ingawa aliwashauri waandaaji wa msafara huo kufikisha msaada wao kwa serikali ya Cyprus, badala ya kuenda moja kwa moja Gaza, ushauri ambao ulikataliwa hapo hapo na waandaaji.

Msafara huo uliopewa jina la Global Sumud Flotila ulitazamiwa kuanza hatua ya mwisho ya safari yake siku ya Ijumaa (Septemba 26) kuingia kwenye Bahari ya Mediterania na kuwasili Gaza.

Angalau mara tatu, msafara huo unaowahusisha wanaharakati kutoka mataifa 52 duniani umeshuhudia mashambulizi ya droni, mara mbili ukiwa nchini Tunisia, na pia kukatwa kwa mawasiliano. 

Waandaaji wa Mashindano ya Eurovision waitisha kura

Waandaaji wa shindano mashuhuri la Eurovision Song Contest walisema siku ya Ijumaa kwamba nchi wanachama “zitapiga kura mwezi Novemba kuamua nchi za kushiriki tamasha hilo mwakani”, kufuatia miito ya kuitaka Israel iondoshwe kutokana na vita vyake dhidi ya Gaza.

Bango la mashindano ya Eurovision.
Bango la mashindano ya Eurovision.Picha: Olesya Kurpyayeva/AFP

Kwa mujibu wa barua pepe iliyotumwa na msemaji wa mashindano hayo, Dave Goodman, “bodi ya wakurugenzi imeshatuma taarifa kwa mataifa wanachama kukutana kwa mkutano wa dharura mapema mwezi Novemba kufanya maamuzi” juu ya suala hilo.

Mataifa kama vile Ireland, Uholanzi, Slovenia na Uhispania tayari yameshatishia kutoshiriki mashindano hayo endapo Israel haitazuiwa.

Urusi ilizuiwa kushiriki tangu mwaka 2022 baada ya uvamizi wake dhidi ya Ukraine .
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *