Katika mkutano huo viongozi mbalimbali wa Afrika wamehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na kushinikiza kuwa bara hilo linapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maamuzi ya kimataifa.
Katika hotuba yake, Rais wa Kongo Denis Sassou Nguesso aliitaja Afrika kama “bara lenye mustakabali mkubwa”, akitaka Umoja wa Mataifa kuwa na “uwakilishi na uwazi zaidi, sambamba na kuwa karibu na uhalisia wa changamoto za ulimwengu. Rais huyo amesema Baraza la Usalama katika muundo wake wa sasa haliakisi tena usawa wa kijiografia wa ulimwengu mzima na kuhimiza mageuzi na Afrika kuwa na kiti cha kudumu.
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadera, alisisitiza katika hotuba yake kwa kusema kuwa Afrika inasubiri ushirikiano wa kishujaa, na kwamba maendeleo jumuishi yanapaswa kutumika kama silaha ya amani na kinga dhidi ya migogoro. “Katika kipindi cha miaka 30 ijayo, mtu 1 kati ya 4 duniani atakuwa Mwafrika,” alisema Touadera.
“Nafasi ya Afrika katika jumuiya ya kimataifa lazima iheshimiwe. Uhuru wa kweli badala ya utegemezi, ushirikiano wa haki badala ya unyonyaji. Ni jambo lisilokubalika kwamba umasikini unaongezeka barani Afrika huku utajiri ukishamiri katika nchi za kaskazini. Ni wakati wa kurekebisha dhuluma zilizofanywa dhidi ya Afrika. Ndiyo maana Jamhuri ya Afrika ya Kati inaunga mkono mpango wa fidia kwa Afrika pamoja na juhudi za bara zima za kuanzisha mazungumzo ya heshima na usawa na washirika,” alisema Rais Touadera.
Mgogoro wa Gaza watawala UNGA
Kando na viongozi hao wa Afrika, wengine waliozungumza ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, António Costa, ambaye amewahimiza viongozi wa dunia kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na migogoro mikubwa duniani. Costa amelaani kile alichokiita “janga la kibinadamu” huko Gaza, akisema kuwa njaa inatumika kama silaha ya vita.
Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza David Lammy ametetea hatua ya nchi hiyo kulitambua taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa. Lammy ameieleza hadhara ya Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi kwamba hali ya Gaza “haikubaliki” na kutetea tangazo la karibuni la Uingereza kutambua rasmi kwa taifa la Palestina.
Naye kiongozi wa Baraza la utawala la Libya Mohamed Younis Menfi amesema watu wa Libya wako tayari kuchukua mkondo wa kidemokrasia baada ya mkwamo wa muda mrefu kuhusu uchaguzi wa kitaifa. Menfi amewaeleza viongozi wa ulimwengu kwamba taifa hilo tajiri kwa mafuta la Afrika Kaskazini “bado lina matumaini, na linaamini katika uwezo wake wa kujenga mustakabali thabiti na wenye mafanikio.”
Pembezoni mwa mkutano huo wa Baraza Kuu, viongozi wa dunia wamekutana kuzindua mazungumzo ya kimataifa kuhusu uendeshaji wa teknolojia ya Akili Mnemba. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameuita mkutano huo kuwa ni “mfano bora wa ushirikiano wa kimataifa.” Majadiliano hayo ya kimataifa yatazingatia athari za AI katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi, kimaadili na kiteknolojia, kitamaduni na kilugha.
Baadae leo, waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kuhutubia Mkutano huo akifuatiwa na viongozi wengine kutoka China, Uingereza, na India.
