Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imemlaani Benjamin Netanyahu na hotuba yake iliyojaa uongo kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, lengo la uongozo huo wa Netanyahu ni kuonesha Muqawama wa Wapalestina ni ushetani na eti Wapalestina wanataka kuwaangamiza Mayahudi lakini uongo huo hautozuia kuendelea Muqawama wa Wapalestina.

HAMAS imesema hayo kwenye taarifa yake maalumu na kuongeza kuwa, madai ya Netanyahu (waziri mkuu wa Israel) ya kwamba Hamas inataka kuwaua Mayahudi kote ulimwenguni ni sehemu ya kampeni yake ya kimfumo ya kuwachafua Wapalestina na Muqawama wao halali wa kitaifa.

Pia imesema: “Harakati ya Hamas na makundi mengine ya Muqawama wa Palestina yamekuwa yakisisitiza mara kwa mara kwamba vita vyao viko tu dhidi ya uvamizi wa ardhi na maeneo matakatifu. Tutaendelea na njia hii hadi taifa la Palestina lipate haki yake ya kujitawala.”

Taarifa ya HAMAS pia imesema kuwa, inashangaza kuona mhalifu wa kivita anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) anaruhusiwa kuhutubia Umoja wa Mataifa kuhusu haki, ubinadamu na uadilifu, huku yeye mwenyewe ndiye mkiukaji mkubwa wa kila siku wa haki za Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza. 

Vilevile imesema, uwongo wa mara kwa mara wa Netanyahu hauwezi kuficha uhakika wa mauaji ya umati na jinai zinazofanywa waziwazi na kiongozi huyo na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Jinai nyingine ni kujaribu kuwalazimisha Wapalestina kuhama makazi yao sambamba na kuwatesa kwa njaa. Mtenda jinai kama huyu hakupaswa kupewa nafasi ya kuhutubia Umoja wa Mataifa.

Hamas pia imebainisha kuwa njama za Netanyahu za kujifanya kuwa anawaonea huruma mateka wa Kizayuni ni mfano wa mawazo ya kikoloni ya mtenda jinai huyo Mzayuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *