Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran ambaye amewasili Beirut kuhudhuria kikao cha Baraza la Kumbukumbu za Mashahidi wa Muqawama wa Hizbullah amesema kwamba, utawala wa Kizayuni hauna huruma na nchi yoyote ile.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Ali Larijani amsema: Moja ya malengo muhimu ya safari yake hiyo ni kuhudhuria kikao kitakachofanyika kuwakumbuka mashahidi wa Lebanon, mashahidi waliojitolea kuilinda na kuipigania Lebanon wakiwemo Shahid Hassan Nasrullah na Shahid Safi al-Din.

Vilevile amesema: Tabia chafu ya utawala wa Kizayuni imebainika zaidi hivi sasa mbele ya mataifa ya dunia. Maneno ambayo Shahid Nasrullah alikuwa akiyasema miongo kadhaa iliyopita sasa ukweli wake umebainika wazi kwa kila mtu.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia amesema: Leo ni wazi kwa kila mtu kwamba utawala wa Kizayuni hauionei huruma nchi yoyote ile. Shambulio la Israel huko Qatar ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo. Ndio maana leo hii nchi tofauti zinatafuta njia za kuwa na ushirikiano wa karibu baina yao ili kujikinga na shari za utawala wa Kizayuni. 

Pia amesema: Iran na Lebanon ni mataifa mawili ambayo yana uhusiano wa kirafiki wa kihistoria. Katika miaka ya hivi karibuni, urafiki kati ya mataifa hayo mawili umeongezeka. Daima Iran imekuwa ikiunga mkono kuwepo serikali zenye nguvu na huru nchini Lebanon.

Amesema: Tunatumai kwamba maendeleo na ustawi wa Lebanon daima utakuwa ni wenye manufaa kwa wananchi Lebanon na utapelekea kuweko serikali zenye nguvu na imara nchini humo zisizokubali kuburuzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *