
Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni zaidi ya miezi tisa tangu Rais huyo wa zamani alipoondolewa mamlakani na kukimbilia Urusi. Jaji Tawfiq al-Ali aliyetangaza hatua hiyo amesema uamuzi wa Syria unatoa nafasi ya kusambaza taarifa kwa polisi wa kimataifa Interpol na kuiendesha kesi hiyo kimataifa.
Assad anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na matukio ya mwaka 2011
Tuhuma zinazomkabili Assad zinahusiana na ukandamizaji uliofanywa na vikosi vyake mwaka 2011 kusini mwa mji wa Daraa. Kipindi hicho, upinzani uliibuka dhidi ya utawala wake ukidai mabadiliko ya kisiasa kwa njia ya amani. Hata hivyo serikali yake iliukabili kwa mabavu na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.