
NILIKUWA nimefadhaika lakini nilijidai kucheka.
“Kwani ukiwa kazini hatuwezi kusalimiana, Hamisa?”
“Juzi uliniambia kwamba unaweza kuchanganyikiwa kama sitakupa jibu haraka. Nimehisi kwamba ndiyo umeanza kuchanganyikiwa. Yaani mimi niache kazi kwa ajili ya kusalimiana na wewe?”
“Sina thamani mbele yako?”
“Hata uwe nayo, lakini niache kuhudumia wagonjwa wangu nianze kuongea na wewe?”
“Nimeona uko kimya sana, Hamisa.”
“Kimya changu kinakukera nini?”
“Leo una nini, Hamisa? Unajua sikuelewi kabisa!”
“Na hutanielewa kwa muda huu. Nipigie nikitoka kazini.”
“Muda gani utatoka kazini?”
Badala ya kunijibu, Hamisa akakata simu. Sikumlaumu. Mwenyewe nilijua nilimuuliza swali la kipuuzi. Siku zote ninaujua muda anaotoka kazini, kwa hiyo aliona upuuzi kunijibu.
Simu ilipokatwa niliitazama kisha nikaiweka juu ya meza.
Hamisa atanitesa sana! Nikajisemea kimoyomoyo.
Lakini nikajiambia ulikuwa wakati wake wa kutamba na kunijibu anavyojisikia kwa vile anajua kuwa ninampenda. Ulikuwa ni wakati wangu wa kuendelea kumrai. Pengine, nilijiambia, ndiyo furaha yake. Waimbaji wa taarab wamesema kuwa “Asiyejua kurai si mlezi wa mahaba.” Na mimi kama mlezi wa mahaba ya Hamisa nitaendelea kumrai hadi dakika ya mwisho, nilijiambia.
Ghafla nikasikia mlio wa meseji kutoka kwenye simu yangu. Nikaishika na kuitazama meseji iliyokuwa imeingia. Ilitoka katika namba ambayo ilikuwa iko akilini mwangu.
Iliandikwa kwa herufi kubwa:
NIMESHATIMIZA ADHABU YA MAHAKAMA ILIYOKUWA IMEKIUKWA YA KUWANYONGA WOTE WALIOTAKIWA KUNYONGWA. SASA NIMERUDI KABURINI.
Ilikuwa meseji iliyonishitua sana. Ilitoka kwa THOMAS CHRISTOPHER. Namba yake ilikuwa ni ile ile niliyoipata kutoka kwenye simu ya Ramadhani Unyeke.
Amenitumia ujumbe kunijulisha kuwa ametimiza adhabu ya kuwanyonga kina Unyeke waliokuwa wamemuua yeye na sasa amerudi kaburini! Nikawaza kwa hofu.
Ina maana kwamba Thomas ni mzuka ulioibuka na sasa umerudi kaburini? Nikajiuliza kwa wasiwasi.
Tutafanya uchunguzi, nikajiambia na hapo hapo nikampigia simu afisa upelelezi ili nimueleze kuhusu ujumbe huo ulionifikia.
Afisa upelelezi alipopokea simu nilimueleza kuhusu ujumbe huo.
“Nitumie kwenye simu yangu,” akaniambia.
“Nitakutumia, lakini unadhani huu ni mzuka kweli?”
“Mzuka?”
“Unajua nimekuuliza hivyo kwa sababu huyu Christopher amethibitika kuwa aliuawa kweli.”
“Kesho tutakwenda kufukua kaburi lake. Mengi tutayajua hapo.”
“Sawa.”
Baada ya hapo nilikata simu nikamtumia mkuu wangu ule ujumbe.
Tukio la kutumiwa ujumbe ule lilinikosesha usingizi usiku.
Asubuhi ya siku iliyofuata, mimi na afisa upelelezi na polisi wanne tulikwenda katika makaburi ya Chuda. Kwanza tulikwenda kwa mwenyekiti wa mtaa ule tukamjulisha juu ya dhamira yetu ya kulifukua kaburi la mtu anayeitwa Thomas Christopher kwa ajili ya uchunguzi wetu.
Mwenyekiti huyo alikubali kufuatana na sisi kwenye eneo hilo la makaburi.
Tulishirikiana kulifukua kaburi hilo hadi tukalipata sanduku lililokuwa ndani, ambalo lilikuwa limeshaoza lakini maiti iliyoanza kuharibika ilikuwemo ndani.
Licha ya uso wa marehemu kutokuwa na hali nzuri, sura yake iliweza kutambulika. Kwa vile nilikuwa na picha yake niliyoipata kutoka kampuni ya simu, tulilinganisha uso na kukubaliana kwamba alikuwa ndiye Thomas Christopher.
Kitu ambacho kilitushitua ni kuwa kwenye dole gumba lake la mkono wa kulia kulikuwa na rangi mbichi ya bluu, rangi ambayo hutumika katika mihuri.
“Huyu ndiye mtu hasa tunayemtaka. Angalia kwenye dole gumba lake kuna rangi ya bluu!” nikamwambia afisa upelelezi.
“Ni rangi ya nini?”
“Umesahau ile alama ya dole gumba aliyokuwa anaiweka kwenye zile karatasi tulizozikuta kwenye shingo za wale watu aliowanyonga?”
Nikamsikia afisa upelelezi akiguna. Nikajua na yeye maji yalikuwa shingoni. Suala hilo lilikuwa limemtatiza japokuwa alikuwa hataki kuamini habari ya mizuka.
Nikaendelea kumtazama afisa huyo ili nijue atasema nini. Nikamuona anatikisa kichwa.
“Ni kitu cha ajabu kwa kweli. Katika hali tunayoiona hapa unaweza kuona hii maiti ndiyo iliyoweka dole katika zile karatasi kwa sababu rangi yenyewe ni mbichi. Hatuwezi kusema kuwa alizikwa nayo,” akaniambia.
“Na kama tutakubali kwamba dole lake ndilo lililotumika katika zile karatasi wakati mwenyewe ni maiti, tutahisi nini, afande?”
Afisa upelelezi alijua kuwa nilikuwa naelekea kwenye imani ya mzuka, akakwepa swali.
“Ni lazima tupime alama za hili dole tulinganishe na ile iliyoko katika zile karatasi tuone kama zinafanana.”
“Sasa nimuite Sajin Ibrahim, mtaalamu wa alama za vidole?”
“Muite.”
Nikatoa simu yangu na kumpigia mtaalamu wetu huyo.
“Hello…” Sajin Meja Ibrahim alisema alipopokea simu.
“Hello Sajin Ibrahim, uko wapi?”
“Niko ofisini.”
“Tafadhali chukua kifaa cha kuchukua alama za vidole ufike hapa Chuda katika eneo la makaburi lililopo nyuma ya shule ya msingi.”
“Nifike muda gani?”
“Ufike sasa hivi, tunakusubiri hapa pamoja na afisa upelelezi.”
“Sawa, ninakuja.”
Haikutimu hata nusu saa, Sajin Meja Ibrahim akawasili. Afisa upelelezi akamuagiza achukue alama za vidole za maiti ya Thomas akazilinganishe na alama zilizoko katika zile karatasi nilizomkabidhi mimi.
Sajin Meja Ibrahim alivaa mipira ya mikononi, akachukua alama za vidole za maiti ya Thomas. Alipokamilisha zoezi hilo tulilifukia kaburi lake kisha tukaondoka.
Tuliporudi kituoni niliingia ofisini kwangu nikajaribu kuipiga ile namba ya Thomas lakini ikawa haipatikani tena. Baada ya kukaa kidogo nilitoka nikaenda kampuni ya simu na kuomba nipatiwe orodha ya namba ambazo ile namba iliwasiliana nazo katika siku za hivi karibuni.
“Unaposema siku za karibuni unamaanisha wiki moja, wiki mbili au muda gani?” mhudumu wa kampuni ya simu akaniuliza.
“Ninamaanisha wiki mbili hivi.”
Mhudumu aliangalia kwenye kompyuta akaniandikia kwenye karatasi namba pamoja na tarehe ilizowasiliana nazo katika muda huo wa majuma mawili ambayo yale matukio ya kunyongwa kina Unyeke yalitokea.
Mhudumu akaniambia katika juma lile, namba ile haikufanya mawasiliano yoyote na simu yake ilizimwa, lakini katika juma lililopita ilifanya mawasiliano na namba mbili tofauti.
Namba hizo zilikuwa ni za Lazaro John na Frenk Unyeke. Wenyewe ndivyo walivyoandikisha majina yao kampuni ya simu.
Nikajua kuwa Thomas aliwasiliana na watu hao kabla ya kuwaua.
“Hebu tazama namba alizowasiliana nazo siku za nyuma,” nikamwambia mhudumu huyo.
“Zipo nyingi.”
“Nipe chache tu.”
Mhudumu akaniandikia namba chache kwenye karatasi na kuniambia:
“Lakini hizo ni za tangu mwaka jana.”
“Ninazihitaji pia.”
Baada ya kupata namba hizo nilitoka. Nilirudi tena ofisini kwangu. Nilianza kupiga namba ya kwanza. Ikaita.
“Hello!” sauti ya mwanamke ikasikika baada ya simu kupokewa.
“Habari yako?” nikamsalimia.
“Nzuri.”
“Samahani, ninaomba kukuuliza kama unamfahamu mtu anayeitwa Thomas Christopher?”
“Thomas Christopher ninayemfahamu mimi alishakufa.”
“Alikufa lini?”
“Nafikiri tangu mwaka jana. Alizikwa Chuda.”
“Nikikwambia mimi ndiye Thomas Christopher utakataa?”
“Wewe ni Thomas Christopher?” sauti ikauliza kwa mshangao.
“Ndiyo, ni mimi.”
Msichana alikata simu hapo hapo. Nikajua nilikuwa nimemshitua nilivyomwambia mimi ni Thomas Christopher wakati anachojua ni kuwa mtu huyo hakuwepo duniani.
Nikaona nimpigie tena ili nimfahamishe ukweli lakini hakupokea. Nilipopiga mara ya pili nikakuta simu yake imezimwa.
Lengo langu lilikuwa ni kutaka kujua watu aliokuwa wanawasiliana na namba ya Thomas walikuwa wanajua kuwa alishakufa au la.
Sasa nikajiuliza: kama watu wanatambua kuwa Thomas alishakufa, inakuwaje aibuke tena na kuwaua wabaya wake?
Ile namba yake iliyokutwa katika simu za watu wawili miongoni mwa aliowaua, ni ushahidi tosha kwamba Thomas ndiye anayeua.
Isitoshe, ujumbe alionitumia kwamba amerudi kaburini baada ya kukamilisha kazi yake ya kuwaua watu hao, na mwili wake kukutwa kaburini siku ile huku dole gumba lake likiwa na rangi mbichi ya bluu kuonyesha kwamba ndiye aliyekuwa akiweka alama za dole kwenye zile karatasi, ni ushahidi mwingine kuwa ni yeye aliyewaua.
Ingawa afisa wangu alikuwa hakubali, lakini mimi niliamini moja kwa moja kwamba Thomas aliibuka tena kama mzuka na kuwaua watu ambao walidhulumu roho yake, na kisha mkuu wa magereza akaacha kuwapa adhabu iliyoamuliwa na mahakama.
Nilikumbuka kwamba zamani babu yangu aliwahi kunipa hadithi ambayo aliniambia ni ya kweli, ya mfalme mmoja ambaye mtoto wake aliwahi kumkanyaga mtoto wa maskini mmoja na kumuua.
Yule maskini alilia kwa uchungu bila hata kupata msaada wowote kutoka kwa mfalme huyo.
Baada ya wiki moja, mfalme aliota yule mtoto wa maskini aliyeuawa akipewa upanga na mtu asiyejulikana na kumwambia: “Na wewe nenda ukamkate kichwa kwa upanga huu yule mtoto wa mfalme aliyekuua.”
Inaendelea…