
Tamasha hilo la muziki, lililofanyika katika bustani maarufu iitwayo Central Park mwishoni mwa wiki ya kilele cha Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, (UNGA) ni tukio kuu la Global Citizen, ambazo ni harakati kubwa zaidi duniani za kukomesha umaskini wa kupindukia.
Mwaka huu, orodha ya wasanii waliotumbuiza ilijumuisha nyota wa kimataifa kama vile Shakira, Cardi B na Rosé.
Safari bado ndefu, tushikamane
Bi. Mohammed alipanda jukwaani kuwashukuru waliohudhuria tamasha hilo na kuwakumbusha kwamba imebaki miaka mitano tu kufikia ukomo wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, (SDGs) – ambayo ni mwongozo wa mustakabali wa haki kwa watu na sayari.
“Bado tuna safari ndefu,” aliwajulisha washiriki wa tamasha hilo huku akisema kuwa, “tunasonga mbele, lakini kasi haitoshi, na kengele inalia kwa nguvu sana.”
Kama Mshauri Maalum wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, Bi. Mohammed alihusika sana katika kusukuma mbele Malengo hayo na kuhakikisha makubaliano miongoni mwa nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.
Akizungumza siku ya Ijumaa, alisisitiza kuwa dola trilioni 4.3 zinahitajika kila mwaka kufadhili Malengo hayo na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Tuone suluhu pale wengine wanapokata tamaa
“Kile kinachojalisha zaidi ni kuipa amani nafasi – kwa wanawake wa Sudan, kwa watoto wa Gaza, kwa watu wa Ukraine. Tunahitaji amani kila mahali,” alisema, akitoa wito kwa kuwepo kwa hatua za kuhakikisha akili mnemba au akili unde haileti mgawanyiko mpya.
Halikadhalika wanawake washirikishwe katika kila meza ya maamuzi, elimu bora, na kulinda sayari, “kuanzia ukanda wa Amazon huko Amerika ya Kusini hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kila pembe ya dunia.”
Naibu Katibu Mkuu huyo alihimiza waliohudhuria kuona suluhisho mahali ambapo wengine wanaona mwisho wa matumaini, na kutumia sauti yao “kupaza kelele, wakidai kila mtu awe bora zaidi na kukataa kuenea kwa hali ya kutojali duniani.”