
Vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa rasmi siku ya Jumapili, Septemba 29 usiku wa manane, kufuatia kushindwa kwa mazungumzo na nchi za Magharibi, ambazo zinadai kuhakikishiwa juu ya mpango wake wa nyuklia. Rais wa Iran amekosoa madai ya Marekani ya kukabidhi uranium “yote” iliyorutubishwa.
Imechapishwa:
Dakika 4 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimerejeshwa leo Jumapili, Septemba 28 usiku a manane, kufuatia kushindwa kwa mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia na nchi za Magharibi, ambazo hata hivyo zimetaka kurejelea njia ya diplomasia. Kwa upande wake, Tehran imefutilia mbali kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, anaripoti mwandishi wetu wa Tehran, Siavosh Ghazi.
“Iran inaonekana imeamua kuanzisha mvutano na nchi za Magharibi. Vikwazo ambavyo viliondolewa haviwezi kurejeshwa,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi. “Nchi za Ulaya ambazo hazijaheshimu ahadi zao hazina haki ya kurejesha tena vikwazo,” ameongeza, akimaanisha utaratibu wa kurejesha vikwazo.
Hakuna nchi inayolazimika kufuata maazimio na vikwazo vya hapo awali vya Umoja wa Mataifa, kulingana na waziri wa mambo ya nje.
Rais wa Iran Massoud Pezeshkian alisema mnamo Septemba 27 kwamba Marekani iliitaka Iran ikabidhi uranium yake yote iliyorutubishwa ili kubadilishana na kuongezwa kwa muda wa miezi mitatu wa kusitishwa kwa vikwazo, na kulitaja ombi hili kuwa “halikubaliki.” “Wanataka tuwape uranium yetu yote iliyorutubishwa,” Massoud Pezeshkian aliambia runinga ya serikali. “Baada ya miezi michache, watakuwa na mahitaji mapya,” rais wa Iran aliongeza.
Tehran inategemea uungwaji mkono wa Urusi na China kukabiliana na kurejeshwa kwa vikwazo kufuatia idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Vikwazo vizito
Mwishoni mwa mwezi Agosti, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani zilianzisha utaratibu wa “snapback”, ambao unaruhusu kurejeshwa kwa vikwazo vilivyoondolewa mnamo mwaka 2015 kufuatia makubaliano ya nyuklia ya Iran ndani ya siku 30. Kufuatia idhni ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kushindwa kwa Urusi na China mnamo Septemba 26 kuongeza muda huo, vikwazo vizito, kuanzia vikwazo vya silaha hadi hatua za kiuchumi, vimerejeshwa.
Vikwazo hivyo vinalenga makampuni, mashirika na watu binafsi wanaochangia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mpango wa nyuklia wa Iran au kutengeneza makombora ya balistiki, ama kwa kutoa vifaa vinavyohitajika, ujuzi au ufadhili. Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuiliwa kwa silaha za kawaida, na kupiga marufuku uuzaji wowote au uwasilishwaji wa silaha kwa Iran. Uagizaji, usafirishaji au uwasilishwaji wa bidhaa na teknolojia zinazohusiana na mpango wa nyuklia na makombora ya balestiki utapigwa marufuku.
Mali ya mashirika na watu binafsi nje ya nchi ambazo ni mali ya watu wa Iran au makampuni yanayohusishwa na mipango ya nyuklia zitazuiwa. Watu walioteuliwa kushiriki katika shughuli zilizopigwa marufuku wanaweza kupigwa marufuku kusafiri ndani ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Nchi hizi wanachama pia zitalazimika kuzuia shughuli za benki na kifedha (utoaji wa huduma, ufadhili) ambazo zinaweza kusaidia Iran katika mipango yake ya nyuklia au makombora ya balestiki. Watu binafsi au makampuni yatakayokiuka masharti haya yatafungiwa mali zao kimataifa.
Matatizo ya kiuchumi
Bunge la Iran limepangiwa kujadili siku ya Jumapili, Septemba 2, iwapo litasalia ndani ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa silaha, kwa mujibu wa mjumbe wa bunge hilo, ambaye ameongeza kuwa bunge hilo pia linaweza kuchunguza suala la utengenezaji wa silaha za nyuklia. Hata hivyo msemaji wa serikali amekiri kuwa kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuliweka aina mpya ya vita dhidi ya Iran na hivyo kufanya hali ya uchumi wa nchi hiyo kuwa ngumu zaidi.
Kushuka kwa sarafu ya Iran kuliendelea Jumamosi, Septemba 27, na kufikia kiwango cha juu zaidi. Pia siku ya Jumamosi, dola moja ilikuwa ikiuzwa kwenye soko lisilo rasmi kwa takriban riali milioni 1.12, rekodi ya juu, kulingana na tovuti kadhaa za ufuatiliaji wa sarafu. Wataalam wanatabiri hali hii itaendelea, na kuchochea mfumuko wa bei, ambao ni zaidi ya 50%.
Diplomasia ilikwama licha ya juhudi
Mikutano ya ngazi ya juu ilifanyika wiki nzima kando ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York katika jaribio la kutafuta suluhu la kidiplomasia. Lakini nchi tatu za Ulaya, ambazo ni Ufaransa, Ujerumani na Uingereza waliamua kwamba Tehran haikutoa “ishara za zinazoonekana.” Nchi hizi za Ulaya ziliweka masharti matatu: kuanza upya kwa mazungumzo na Marekani, kufikia wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kwenye maeneo nyeti ya nyuklia ya Natanz, Fordo, na Isfahan, yaliyoshambuliwa mwezi Juni na Israel na Marekani, mchakato kwa ajili ya kuhifadhi uranium iliyorutubishwa.
Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimekaribisha kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran kutokana na mpango wake wa nyuklia siku ya Jumapili, Septemba 28. “Tunaitaka Iran ijiepushe na hatua zozote za kuongezeka na kurejea kutekeleza majukumu yake,” Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa waliandika katika taarifa yao ya pamoja. Nchi hizo tatu “zitaendelea kufanya kazi na pande zote kutafuta suluhu la kidiplomasia ambalo litahakikisha Iran haipati kamwe silaha ya nyuklia,” wameongeza.