Kenya imepiga hatua kubwa katika kupanua maandalizi ya kidijitali. Kufikia mwaka 2023, asilimia 82 ya shule za msingi za umma zilikuwa zimeunganishwa na umeme kupitia gridi ya taifa, na asilimia 14 nyingine kupitia nishati ya jua.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya shule 22,800 zilipatiwa vifaa vya kidijitali milioni 1.17, ingawa shule 216 pekee ndizo zilizo na mtandao wa intaneti wa kuaminika.

Ann Kibara, mwalimu mkuu wa shule ya Ng’ando, jimbo la Machakos.

“Tumepiga hatua kubwa kutumia teknolojia kwa sababu tunatumia mfumo wa kurusha picha kufunza, vipakatalishi na redio. Wanafunzi wanakumbuka zaidi wanapotumia teknolojia ikilinganishwa na kufundishwa moja kwa moja. Tunafunza kutoka shule ya chekechekea hadi ya msingi.” alisema Ann Kibara, mwalimu mkuu wa shule ya Ng’ando, jimbo la Machakos.

Zaidi ya wanafunzi Milioni 2.26 waliathiriwa na mabadiliko ya tabianchi wakati wa mafuriko ya mwaka 2024, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwa na mifumo ya elimu inayostahimili misukosuko. Mpango wa Kisekta wa Elimu wa Kitaifa wa Kenya (2023–2027) unalenga mageuzi ya kimsingi, ikiwemo kuanzishwa kwa Vituo vya Rasilimali za Elimu kusaidia wanafunzi wote, wakiwemo wale wanaoishi na ulemavu.

Moureen Kabuchi, afisa kutoka shirika la Action Foundation.

“Ubunifu wetu ni kupitia basi la maktaba lililo na vifaa vya kisayansi, ili kuwapa fursa wanafunzi wanaoishi na ulemavu kupata elimu ya kiteknolojia mahali walipo. Tulianza mwaka uliopita na tumewafikia wanafunzi 2,700 katika shule 35 maalumu, tukiwafunza masomo ya kisasa kama roboti na kuboresha uzoefu wao wa kutumia teknolojia.” Alieleza Moureen Kabuchi, afisa kutoka shirika la Action Foundation.

Faith Nduchi ni mtaalam wa teknolojia kutoka shirika la EdTech.

“Tumekuwa na hali nzuri ya teknolojia katika elimu, ilianza na uwekezaji kutoka kwa serikali kwa shule, kufundisha walimu, na kampuni nyingi zimetengeneza mifumo kusaidia madarasa, kama kusahihisha kwa haraka.” Alisisitiza Faith Nduchi ni mtaalam wa teknolojia kutoka shirika la EdTech.

Mkutano wa Kitaifa wa EdTech 2025 lina malengo ya  kuunda sera, kutatua changamoto zilizopo, na kuhakikisha mfumo wa elimu wa Kenya unatoa masomo ya kisasa, jumuishi na salama kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *