Muda unakimbia: Mkataba wa kibiashara kati ya Marekani na nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ujulikanao kama AGOA (African Growth and Opportunity Act), unamalizika tarehe 30 Septemba. Baada ya mashaka ya muda mrefu kuhusu kuendelezwa kwake, mkataba huu wa miaka 25 uliotoa nafasi ya kuuza bidhaa bila ushuru kwenye soko la Marekani, unaweza kuwa historia.

“Utafiti unaonyesha kuwa AGOA ilikuwa na faida. Mauzo ya nje kuelekea Marekani yaliongezeka, hasa katika sekta ya nguo,” anasema Zoryana Olekseyuk, mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Maendeleo na Uendelevu (IDOS).

Athari kwa Afrika ni ndogo

Hata hivyo, Olekseyuk anaona matokeo yake ni ya mchanganyiko: “Athari kwa jumla katika ukanda huu zilikuwa ndogo na zilitofautiana kati ya nchi na sekta. Kadri muda ulivyopita, washirika wengine wa biashara walipewa kipaumbele zaidi.”

Ushirikiano huu ulianzishwa mwaka 2000 chini ya Rais Bill Clinton. Lakini kurejea kwa Donald Trump Ikulu mwaka 2025 kulirudisha siasa za kulinda bidhaa za ndani na ushuru mkubwa wa kimataifa — hali inayomaanisha pia mwisho wa AGOA.

Eunice Wanjiru anachambua kuhusu AGOA, mpango wa kibiashara kati ya Marekani na Afrika.
Mpango wa AGOA unaziwesha nchi za Afrika zinazotimiza vigezo kuuza bidhaa zake nchini Marekani pasina kutozwa ushuru.Picha: DW

Kwa sasa, nchi 35 za Afrika zinanufaika kupitia AGOA: karibu bidhaa 7,000 zinaruhusiwa kuuzwa Marekani bila ushuru. Sekta kama nguo, kilimo na madini zilipata maendeleo, na ajira nyingi ziliundwa hasa katika mataifa kama Madagascar, Lesotho na Afrika Kusini.

Sasa mafanikio haya yako hatarini. Malick Sané, mtaalamu wa biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop, anasema: “Makampuni ya Kiafrika yatapata ugumu mkubwa kuendelea kushindana kwenye soko la Marekani.” Hii inaweza kupunguza uzalishaji na ajira.

Afrika Kusini, ambayo ndiyo msafirishaji mkubwa zaidi wa bidhaa Marekani, inahofia kupoteza zaidi ya ajira 35,000 katika sekta ya machungwa pekee. Marekani pia imeweka ushuru kwenye mauzo ya platinamu, dhahabu, almasi na madini adimu — vyanzo muhimu vya mapato kwa nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Lesotho, Namibia na Madagascar. Madagascar sasa inalazimika kulipa kodi ya asilimia 47 kwa vanila na nguo.

Lesotho, inayojulikana kwa utengenezaji wa jeans, ilitishiwa na ushuru wa rekodi wa asilimia 50, ambao baadaye ulipunguzwa hadi asilimia 15. Mauritius itatozwa asilimia 40 kwa bidhaa zake za viwandani. Hata hivyo, baadhi ya malighafi hizi bado haziepukiki kwa viwanda vya Marekani.

Faida za kibiashara zilikuwa ndogo

Lakini utafiti unaonyesha biashara na Marekani tayari ilikuwa ikipungua. “Tangu 2017, ni asilimia 8.5 pekee ya mauzo ya nje kutoka nchi za AGOA yaliyokwenda Marekani — chini sana kuliko Ulaya au China,” anasema Olekseyuk. Aidha, wachache tu walinufaika na AGOA kwa sababu faida hazikuwa kubwa vya kutosha.

Afrika Kusini | Mkataba wa Ukuaji na Fursa za Afrika | AGOA
Wajumbe wakihudhuria ufunguzi wa jukwaa la biashara kati ya Marekani na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kujadili mustakabali wa Mpango wa AGOA, jijini Johannesburg, Afrika Kusini, Novemba 3, 2023.Picha: SIPHIWE SIBEKO/REUTERS

Kutokana na hali hiyo, mara nyingi haikuwa na maana kulipa gharama za taratibu za AGOA. Pia kulikuwa na hali ya kutokuwa na uhakika — mara kwa mara ilihitaji kuongezwa muda, baadhi ya nchi zikafungiwa, na wawekezaji wakaogopa.

Baadhi ya nchi kama Zimbabwe ziliondoa vizuizi vya ushuru ili kupunguza shinikizo. Nchi kama Afrika Kusini na Madagascar zinaendelea kuomba masharti ya kipekee.

Fursa ya kihistoria: Kujitoa kwenye utegemezi

Mchumi kutoka Mali, Etienne Fakaba Sissoko, anaona huu ni wakati wa mabadiliko: “Nchi zinapaswa kutumia fursa hii ya kihistoria kujitoa kwenye utegemezi. Kwa miaka 25, AGOA imeonekana kama zawadi, lakini ukweli ni kwamba imewasaidia zaidi Marekani.”

Anasema AGOA ilifungua nafasi lakini haikubadilisha uchumi. “Mwisho huu lazima utumike kama hatua ya kutoka kwenye utegemezi hadi kujitegemea.” Anaongeza kuwa changamoto kubwa ni kuwekeza kwenye miundombinu na teknolojia.

Umoja wa Afrika umekuwa ukisukuma kuimarishwa kwa Eneo la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA) lililoanza 2021, ili kujenga uhuru wa kiuchumi. AfCFTA, inayojumuisha nchi 54 na watu bilioni 1.55, sasa inaweza kuwa kivutio kikubwa kwa biashara.

Wakati huo huo, ushirikiano mpya unazidi kujengeka: China, ambayo imeondoa ushuru kwa nchi 33 za Afrika, inajitokeza kama mbadala. Umoja wa Ulaya pia unabaki mshirika muhimu kupitia makubaliano ya kiuchumi, huku India, Uturuki, Brazil na Urusi nazo zikiongeza ushawishi.

Kenya | Ujumbe wa video kutoka kwa Obama katika Mkutano wa Mkataba wa Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA)
Ujumbe wa aliekuwa Rais wa Marekani Barack Obama ukioneshwa kwenye skirini wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nane wa AGOA, mjini Nairobi, Kenya, Agosti 5, 2009.Picha: Sayyid Azim/AP/picture alliance

Ushirikiano mpya kuimarishwa

Mamady Kamara, mshauri wa sera na ujasiriamali, anasema Afrika haina budi kuendelea kupanua ushirikiano wake. Lakini anatahadharisha: “Changamoto ni kutoangukia utegemezi mpya, bali kujadiliana mikataba yenye usawa inayosaidia thamani kuongezeka ndani ya nchi zetu.”

Kwa sasa, swali ni: Mwisho wa AGOA utaathiri vipi bara la Afrika? Mwaka 2024, mauzo ya nje kupitia mkataba huu yalifikia dola bilioni 8. Wakati huohuo, biashara kati ya China na Afrika ilipanda kwa asilimia 4.8 kufikia dola bilioni 295.

Athari zitahisiwa zaidi katika nchi zinazouza sehemu kubwa ya bidhaa zao Marekani, kama Afrika Kusini (dola bilioni 3.76), au zile zinazoitegemea Marekani kwa kiwango kikubwa, kama Lesotho, Madagascar, Botswana na Chad. Hii inaweza pia kupunguza uwekezaji, kudhoofisha minyororo ya usambazaji, kuongeza umaskini na matatizo ya kifedha.

Kwa Olekseyuk, ujumbe wa mwisho ni wazi: “AGOA ilikuwa muhimu, lakini haivutii tena. Mwisho wake unaonyesha zaidi haja kubwa kwa Afrika kubadili na kupanua ushirikiano wake wa kibiashara — na Ulaya ina wajibu wa kusaidia mabadiliko haya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *