
Amesisitiza kuwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Shirika la kimataifa lililoundwa baada ya Vita Kuu vya Kwanza 1919 League of Nation na Kusainiwa kwa Mkataba wa Versailles, lengo lake likiwa kuhakikisha amani ya dunia, kushughulikia migogoro kati ya mataifa, na kuzuia vita zaidi hayajafanikisha malengo yake ya awali.
“Kwa hakika, mifumo ya zamani na ya sasa ya dunia imejikita katika ukiritimba, ujambazi, na udanganyifu,” amesema, akisisitiza kuwa nguvu za kijeshi, mifumo ya kifedha, na hata propaganda zimekuwa zikitumika kudhibiti mataifa dhaifu.
Hali ya Kiuchumi ni mbaya barani Afrika
Akielekeza hotuba yake Afrika, Saleh ameeleza taswira ya uchumi duni na unyonyaji. “Asilimia kubwa ya uchumi wa Afrika umesalia kuwa wa kiasili,” amesema, akielezea jinsi malighafi zinavyouzwa kwa bei ndogo huku bidhaa zilizokamilika zikiletwa kuuzwa kwa bei za juu.
Amelaani ufisadi, kuhamia kwa wataalamu barani Afrika Kwenda kusaka maisha bora na madeni yanayoongezeka, akionya kuwa bara hilo linakabiliana na “ongezeko la haraka la idadi ya watu pamoja na changamoto na majanga yanayokaribia.”
Kwa mujibu wake, hali ya Afrika ni mfano wa ukosefu wa haki wa mfumo wa dunia ulioundwa kuongeza utajiri kwa wachache kwa gharama ya wengi.
Amesema, “Afrika inasalia kuwa bara ambalo malighafi huuzwa nje kwa zile zinazoitwa nchi zenye uchumi ulioendelea kwa bei ndogo, na bidhaa za viwandani zilizokamilika huingizwa kwa bei zilizopandishwa bei sana, ambapo nchi hizi zinasumbuliwa na hasara kubwa katika fursa za ajira, na ambapo rasilimali watu na nguvu kazi ndogo ya wataalamu na wenye ujuzi inatoroshwa kwa sababu ya uhamiaji na uchukuaji wa wataalamu.”
Na zaidi ya yote akasema, Afrika “ ni bara ambalo tawala zinazoongoza hutumia hovyo pesa za mkopo lakini kwa ujanja huonesha dalili za maendeleo huku zikilemewa na deni linaloongezeka; zinajihusisha na ufisadi na utumwa wa kisiasa kwa mataifa ya nje, zinasumbuliwa na kuyumba kwa sababu ya mgawanyiko wa ndani na migogoro ya kudumu.”
Wito wa kuondolewa vikwazo kwa Eritrea na Cuba
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Eritrea amelaani vikwazo vya pande moja kama zana za ukandamizaji. “Tunaomba kuondolewa kikamilifu kwa vikwazo vyote vya upande moja vilivyowekwa dhidi ya nchi kama Eritrea na Cuba, ikiwa ni pamoja na vikwazo visivyo vya haki vya Cuba vilivyodumu kwa miaka 60”.
Saleh ameelezea hatua hizo kama zisizo halali na zenye kuharibu matarajio ya msingi ya nchi zinazotafuta amani, ustawi, na usawa.
Matamanio ya binadamu: Amani, ustawi, na haki
Saleh amelikumbusha Baraza Kuu kuwa matamanio ya msingi ya binadamu hayajabadilika, umiliki wa rasilimali, amani na utulivu, haki, heshima ya pande zote, na uongozi unaofaa.
Amesema “Ingawa matamanio ya binadamu hayajafanikishwa bado, matamanio haya muhimu hayawezi kuwekwa kando au kuahirishwa,”. Kushindwa kuyafanikisha, amesema, kunazidisha tu “dharura ya kimaadili ya kupinga ukosefu wa haki na kusukuma mfumo wenye usawa zaidi.”
Wito wa mshikamano wa kimataifa na umoja wa Afrika
Mwisho, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Eritrea ameyataka mataifa, hasa barani Afrika, kuimarisha uratibu na mshikamano wao. Amesema “Kazi ya haraka na ya muhimu kwa watu wote duniani ni kuimarisha mashirika yao na mifumo ya uratibu ili kushinda ukosefu wa haki wa muda mrefu,”
Saleh amesisitiza wajibu wa Afrika kuchangia “kwa nguvu zaidi katika kuunda mpangilio mpya wa dunia unaoweka mbele haki, usawa, na maendeleo ya pamoja.”