Jeshi la Sudan (SAF) limetangazaa kuwa limepata ushindi mkubwa katika mapambano yake na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika eneo la Kordofan, huko Magharibi mwa Sudan. Hata hivyo RSF wamekanusha madai hayo.

Katika taarifa yake, Jeshi la Sudan SAF linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Al Burhan limesema kuwa, SAF imepata ushindi mkubwa kwenye operesheni zake katika jimbo la Kordofan Kaskazini, ikiwa ni pamoja na kuua mamia ya wanamgambo, kuteka zaidi ya magari 100 ya kivita na kukomboa maeneo kadhaa.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito la Sudan ambaye pia ni kamanda mkuu wa SAF, alitembelea mji wa kimkakati wa Bara, ambao jeshi la Sudan SAF linasema kuwa liliuteka tarehe 11 mwezi huu wa Septemba.

Taarifa zinasema kuwa mapigano makali yanaendelea tangu Ijumaa usiku kati ya SAF na RSF kwenye viunga vya magharibi mwa El Obeid, makao makuu ya jimbo la Kordofan Kaskazini.

Kwa upande wake, RSF imesema kuwa imefanikiwa kuzima shambulio lililoongozwa na SAF kwenye maeneo mengi huko magharibi mwa mji wa El Obeid.

Sehemu moja ya taarifa ya RSF imesema: “Tumesababisha hasara kubwa kwa wapiganaji na zana za kivita za vikosi vilivyotushambulia. Vikosi vyetu vimeendelea kubakia imara katika nafasi zao na vimedhamiria kusonga mbele kuelekea kwenye maeneo mapya ili kujiandaa kwa ajili ya mapigano makali zaidi dhidi ya ngome za adui.”

Tangu Mei 10, 2024, mapigano makali yamekuwa yakiendelea huko El Fasher kati ya SAF na washirika wake kwa upande mmoja, na RSF kwa upande mwingine. Mapigano yamezidi kuwa makali katika siku za hivi karibuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *