
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Ameer Ahmed
- Nafasi, BBC World Service
Moyo wenye afya ni muhimu sana kwa uhai wa mwili wako.
Moyo hupiga na kusukuma damu, ambayo husafirisha hewa ya oksijeni na virutubisho muhimu mwilini.
Bila moyo kufanya kazi vizuri, viungo vingine vya mwili haviwezi kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya moyo na mishipa ya damu (Cardiovascular diseases – CVDs) ndiyo chanzo kikuu cha vifo duniani, yakisababisha vifo vya karibu watu milioni 18 kila mwaka.
Kati ya hao, vifo vinne kati ya vitano husababishwa na mshituko wa moyo au kiharusi.
Kulingana na madaktari bingwa wa moyo, uwezo wa mtu mzima kuwa na mapigo ya moyo ya kupumzika kati ya 60 hadi 100 kwa dakika ni ishara ya moyo mzuri.
Daktari bingwa wa moyo kutoka Marekani, Dkt. Evan Levine, anasema:
“Tunaweza kulinda moyo wetu mapema maishani kwa kula vizuri, kufanya mazoezi, na kuepuka bidhaa za tumbaku.”
Lakini je, moyo mzuri unamaanisha huwezi kupata mshituko wa moyo? Ili tuelewe hilo, kwanza tujiulize.
Mshituko wa moyo ni nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshituko wa moyo (Heart attack) hutokea pale ambapo usambazaji wa damu kwenda kwenye moyo unazibwa ghafla.
Kadri damu isivyofika kwenye moyo, misuli ya moyo huanza kuharibika au kufa.
Bila matibabu ya haraka, sehemu ya moyo inaweza kuharibika kabisa.
Ikiwa sehemu kubwa ya moyo itaathirika, moyo huacha kupiga kabisa hali inayojulikana kama mshtuko wa moyo wa ghafla (cardiac arrest), na mara nyingi husababisha kifo.
Nusu ya vifo vya mshituko wa moyo hutokea ndani ya masaa matatu hadi manne baada ya dalili kuanza, ndiyo maana ni muhimu kutibu dalili hizi kama dharura ya kiafya.
Sababu kuu ni ugonjwa wa moyo wa mishipa (coronary heart disease) ambapo mafuta (plaki) hujikusanya kwenye mishipa ya damu, na kuifanya kuwa myembamba hadi damu inashindwa kupita kwa urahisi.
Kila mwaka, watu wapatao 805,000 nchini Marekani hupata mshituko wa moyo, ambapo 605,000 ni mara yao ya kwanza, na 200,000 ni waliopata tena.
Kwa wastani, mtu mmoja hupata mshituko wa moyo kila sekunde 40 (kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani – CDC).
Jinsi ya kutambua dalili za mshituko wa moyo

Chanzo cha picha, Getty Images
Dalili tofauti hutokea kwa watu tofauti, lakini ya kawaida ni maumivu ya kifua sio tu maumivu makali, bali mashinikizo au kubanwa sana kifuani.
Kwa wanawake, maumivu ya kifua yanaweza kuambatana na maumivu kwenye shingo, mikono yote miwili, mgongo au taya.
Dkt. Ailin Barseghian, daktari wa moyo kutoka California, anasema:
“Wakati mwingine, watu huchanganya mshituko wa moyo na kiungulia (indigestion). Lakini tofauti ni kuwa, maumivu ya mshituko wa moyo husambaa hadi mkono wa kushoto, taya, mgongo au tumbo.”
Dalili nyingine ni:
- Kuhisi kizunguzungu au kudhoofika
- Kutokwa jasho kupita kiasi
- Kupumua kwa shida au kwa sauti (wheezing)
Wakati mwingine dalili huanza masaa au siku kabla ya tukio. Ikiwa una maumivu ya kifua yasiyopungua kwa kupumzika hiyo ni ishara ya hatari.
Dkt. Barseghian anashauri:
“Baada ya saa tatu, misuli ya moyo huanza kufa. Tumia tembe ya aspirini huku ukisubiri huduma ya dharura.”
Madaktari wa moyo wanasisitiza kupata matibabu mara moja ikiwa unafikiri unaweza kuwa na mshtuko wa moyo.
“Jua hali yako: umri, uzito, historia ya familia, kama unavuta sigara au unakunywa pombe. Ukiona dalili, hasa shinikizo kifuani, piga simu kwa huduma ya dharura mara moja.” Usisite. Daktari Levine anasema.
Watafiti wameonya kuwa magonjwa ya moyo mara nyingi huchukuliwa kama ‘magonjwa ya wanaume’, jambo linalosababisha wanawake kutoshirikishwa vya kutosha katika tafiti na hivyo kutopata matibabu bora kwao.
Utafiti uliohusisha watu karibu 300,000 nchini Uingereza, ulionyesha wanawake, watu weusi, na wanaoishi katika mazingira duni, walikuwa na nafasi ndogo ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, na walikufa au kurudi hospitalini ndani ya mwaka mmoja baada ya upasuaji.
Vitu kama shinikizo la damu, uvutaji sigara, na kisukari huongeza hatari kwa wanawake zaidi kuliko wanaume.
Jinsi ya kuzuia mshtuko wa moyo

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna njia kadhaa za kupunguza hatari yako ya kupata mshtuko wa moyo, kama vile:
- Kupunguza shinikizo la damu
- Kudhibiti lehemu (cholesterol)
- Mazoezi ya mara kwa mara
- Lishe bora
Lehemu ni mafuta yanayopatikana kwenye damu. Ingawa ni muhimu kwa mwili, kiwango kikubwa cha aina mbaya ya lehemu huongeza hatari ya magonjwa ya moyo.
Lishe bora ni pamoja na:
- Chakula chenye mafuta kidogo na nyuzinyuzi nyingi
- Kupunguza chumvi hadi si zaidi ya gramu 6 kwa siku
Kuepuka vyakula vyenye mafuta yaliyojaa kama:
- Mikate yenye nyama
- Keki na biskuti
- Siagi
- Vyakula vyenye mafuta ya mawese
Badala yake, kula vyakula vyenye mafuta yasiyojaa, kama:
- Samaki wenye mafuta (kama salmon)
- Parachichi
- Karanga
- Mafuta ya mboga
“Lishe ya Mediterania ni nzuri sana, imethibitishwa kisayansi kupunguza magonjwa ya moyo.” anasema Dkt. Barseghian,
Kufanya mazoezi na kudumisha uzito bora ni njia muhimu ya kudhibiti shinikizo la damu na kuweka moyo katika hali nzuri.
Dkt. Levine anashauri:
“Fanya mazoezi angalau dakika 30, mara tano kwa wiki. Lakini usivute sigara kamwe wala kuvuta vape.”
Utafiti unaonyesha watu 24,097 wanaotumia sigara za kawaida na zile za kielektroniki (e-cigarettes) wanapata madhara sawa ya moyo. Ingawa wale wanaotumia e-cigarette peke yao huwa na hatari ndogo kwa asilimia 30–60%, bado kuna madhara.
Kama tayari umeshapata mshituko wa moyo, takriban asilimia 20 ya wagonjwa hurejea hospitalini ndani ya miaka mitano kwa tukio jingine.
Dawa za kupunguza lehemu kama statins na ezetimibe husaidia kupunguza hatari hiyo, kulingana na watafiti wa Imperial College London na Chuo Kikuu cha Lund, Uswidi.
“Tuna miaka mingi ya ushahidi kwamba kadri LDL cholesterol inavyoshuka, ndivyo hatari ya magonjwa ya moyo inavyopungua,” anasema Dkt. Barseghian.
Kuongezeka kwa vijana wenye mashambulizi ya moyo

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa zamani mshituko wa moyo ulionekana kuwa wa wazee, sasa unaongezeka miongoni mwa vijana.
Mwaka 2019, asilimia 0.3 ya watu wenye umri wa miaka 18–44 walipata mshituko wa moyo. Lakini ifikapo 2023, idadi hiyo imeongezeka hadi 0.5%.
Dkt. Levine anahusisha ongezeko hili na:
- Kula vyakula vilivyosindikwa
- Kukosa kufanya mazoezi
- Mtindo wa maisha usiofaa baada ya COVID-19
Pia ”watu wanaofanya kazi kutoka nyumbani wanajenga maisha ya uvivu na yasiyo na afya,” anasema Dkt. Evan Levine.
Ingawa uvutaji sigara unatambuliwa wazi kama chanzo cha atherosclerosis (kujikusanya kwa mafuta kwenye mishipa), madaktari wa moyo kama Dkt. Levine wana wasiwasi mkubwa pia kuhusu athari za vape kwa vijana.
“Bado hatujajua kikamilifu madhara ya muda mrefu ya kuvuta e-cigarettes, lakini dalili zinaonyesha si salama,” anaonya.
Dkt. Ailin Barseghian anaongeza kuwa kuna sababu nyingine zinazoweza kuongeza hatari ya kupata mshituko wa moyo ukiwa bado kijana, kama vile:
- Magonjwa ya kurithi ya lehemu nyingi (familial hyperlipidaemia)
- Msongo wa mawazo
- Kutopata usingizi wa kutosha au usingizi wa shida
“Sababu za kimazingira kama msongo na usingizi mbaya zinazidi kutambuliwa kama vihatarishi vya moyo,” anasema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid