
Akihutubia Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 hii leo mjini New York Marekani amesema “Niruhusu nisisitize kauli ya mara kwa mara ya Rais Hakainde Hichilema kwa dunia kwamba ukosefu wa utulivu kokote kule ni ukosefu wa utulivu kila mahali.”
Amesema Zambia inaendelea kusaidia jitihada za upatanisho na ulinzi wa amani za Umoja wa Afrika, hasa katika Pembe ya Afrika na Kanda ya Maziwa Makuu, akiwataka wanajamii ya kimataifa kusaidia “kufanya silaha kimya” barani Afrika.
Ametumia pia hotuba yake kuzungumzia elimu Zambia akisema kuwa, “Kwa kuamini kwamba elimu ndiyo njia kuu ya kusawazisha fursa, serikali yetu ilianzisha elimu ya msingi na sekondari bila malipo kwa watoto wote, na ikaajiri idadi kubwa ya walimu ili kuboresha ubora wa elimu.”
Pia Waziri huyo amesisitiza mshikamano mpya wa kimataifa na mageuzi ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Akizungumza kwa niaba ya Rais Hakainde Hichilema, Haimbe amesisitiza kuwa amani, maendeleo, na haki za binadamu lazima ziwe katika msingi wa kazi za Umoja wa Mataiifa.
“Uchaguzi wa kaulimbiu Kwa pamoja tu bora zaidi, Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu,’ ni wa wakati unaofaa kwani inasisitiza hitaji la kushirikiana kwa maslahi ya pamoja,” Haimbe. Amethibitisha imani ya Zambia katika Chata ya Umoja wa Mataifa kama msingi wa amani na ushirikiano wa kimataifa, akibainisha kuwa Umoja wa Mataifa umefanikiwa “kusaidia kuzuia migogoro mikubwa, kuendeleza ukoloni, na kuchukua nafasi ya uongozi katika afya ya umma, elimu, na misaada ya kibinadamu iliyoookoa maisha ya maelfu kwa mamilioni ya watu.”
Mageuzi ya ndani, maendeleo na tabianchi
Haimbe ameonesha mageuzi ya ndani ya Zambia yaliyoanzishwa kuboresha rasilimali za binadamu. Serikali imeanzisha elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kupanua upatikanaji wa huduma za afya, na kuimarisha mifumo ya msaada wa kijamii, ambapo mpango wa ugawaji wa fedha za kijamii au Social Cash Transfer sasa unafikia zaidi ya 6.5% ya kaya.
“Tukiamini kuwa elimu ni kigezo kikubwa cha usawa, serikali yetu imeajiri walimu idadi kubwa zaidi ili kuboresha ubora na upatikanaji wa elimu,” amesema akiongeza kuwa wanawake na vijana wako katikati ya mageuzi ya Zambia kupitia hatua za uhakika, sheria za kupinga ukatili wa kijinsia, na kampeni za kuondoa ndoa za utotoni.
Ameendelea kusema kuwa Zambia inaendelea kurejesha utulivu wa kiuchumi kupitia marekebisho ya madeni na mpango unaosaidiwa na Shirika la Fedha Duniani IMF.
Haimbe pia ameonya kuhusu tishio la haraka la mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na athari kubwa licha ya mchango mdogo katika uzalishaji wa gesi chafuzi. “Tunahitaji kuchukua hatua sasa, kupunguza ongezeko la joto duniani na kuendana na athari zake. Hebu tuhamasishwe kuchukua hatua za kishujaa zinazolinda sayari kwa vizazi vijavyo,” amewaambia nchi wanachama huku akijiandaa kuelekea COP30 nchini Brazil.
Wito la Mageuzi ya UN na uwakilishi wa Afrika
Akizungumza juu ya muundo wa Umoja wa Mataifa, Haimbe amekaribisha Mpango wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa wa UN80, unaolenga kuboresha ufanisi na utendaji, lakini akasisitiza kuwa mageuzi hayapaswi kupunguza msaada kwa nchi zinazoendelea.
Amebainisha kuwa ukosefu wa haki wa kihistoria wa Afrika kutokuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama, akithibitisha kuwa Zambia inaunga mkono msimamo wa pamoja wa Afrika kuhusu Mageuzi ya Baraza la Usalama.
“Maamuzi kuhusu masuala muhimu ya amani na usalama mara nyingi yanakwama kutokana na nguvu ya veto ya wachache, hata pale wanachama wengi wanaposema wazi,” amesema.
Akimalizia hotuba yake, Haimbe ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kwa pamoja na kwa ujasiri. “Miaka themanini iliyopita, dunia ilitoka kwenye vita na ahadi ya kutoruhusu tena mgawanyiko na uharibifu kuamua mustakabali wetu wa pamoja. Hebu kikao hiki cha 80 cha Jumuiya ya kiataifa kikumbukwe kama hatua ya mabadiliko ambapo dunia ilichagua mshikamano badala ya kimya, haki badala ya kutokuwa na hatua, na umoja badala ya mgawanyiko,” amesema.
Ameongeza kuwa Zambia inaendelea kujitolea kwa ushirikiano wa kimataifa, amani, na maendeleo endelevu huku jumuiya ya kimataifa ikikabiliwa na changamoto zisizo za kawaida.