Kampeni zimeanza rasmi mwishoni mwa jumaa lilopita huku rais na mgombea wa chama tawala Paul Biya akiwa hayupo nchini humo. Paul Biya mwenye umri wa miaka 92, ndiye rais mkongwe zaidi duniani na ameitawala Cameroon tangu mwaka 1982 na sasa anawania muhula wa nane madarakani. Lakini hakuwepo nchini jana Jumapili wakati kampeni zikipamba moto kuelekea uchaguzi huo utakaoamua nani atakayechukua nafasi hiyo.
Kulingana na ofisi yake, Paul Biya aliondoka Cameroon wiki moja iliyopita katika kile kilichotajwa kuwa “safari binafsi” kuelekea barani Ulaya. Lakini duru za kidiplomasia zinasema kiongozi huyo ambaye ni nadra kuonekana hadharani yupo mjini Geneva, Uswisi. Rais huyo hakuhutubia alhamisi iliyopita mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kama ilivyopangwa na aliwakilishwa na waziri wake wa mambo ya nje.
Wagombea watangaza sera zao
Kampeni za uchaguzi zilianza Jumamosi na kuendelea Jumapili huku wapinzani wakuu wa Biya wakifanya mikutano kadhaa. Cabral Libii, mgombea wa chama cha upinzani cha Cameroon Party for National Reconciliation (PCRN), alikutana na wafuasi wake katika mji wa pwani wa Douala akisema kuwa uchaguzi huu ni muhimu sana:
“Uchaguzi huu, ni uchaguzi wa kuelezea ghadhabu; haufanani na chaguzi zingine zilizotangulia. Ni uchaguzi ambao lazima tuchague kati ya maisha na kifo. Lazima tuchague kati ya mpasuko au muendelezo.”
Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa utalii, Bello Bouba Maigari aliwakusanya mamia ya wafuasi wa chama cha National Union for Democracy and Progress akishirikiana na mgombea mwingine, Akere Muna, ambaye alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono Bouba Maigari.
Paul Biya akabiliwa na ukosoaji
Biya ambaye ameiongoza Cameroon kwa miaka 43 , anapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo kutokana na mgawanyiko ndani ya upinzani, hajawahutubia moja kwa moja raia wa Cameroon tangu Julai 13, alipotangaza kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa anagombea tena urais. Mnamo Septemba 17, 2025, binti wa rais bi Brenda Biya alichapisha video kwenye mtandao wa TikTok akiwatolea wito raia wa Cameroon kutompigia kura baba yake. Baadaye aliifuta video hiyo na kuomba samahani.
Utawala wa Biya umekuwa ukikosolewa kwa vitendo vya kukandamiza upinzani pamoja na ufisadi. Uchunguzi wa mwaka 2018 kuhusu uhalifu wa kiuchumi uliofanywa na muungano wa waandishi wa habari uligundua kuwa Paul Biya alitumia takriban miaka 4.5 ya uongozi wake akiwa nje ya nchi, haswa nchini Uswisi, kwa gharama inayokadiriwa kufikia dola milioni 65.
//AFP